Na Said Mwishehe,Michuzi TV- Same
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan akiwa wilayani Same mkoani Kilimanjaro amesema Serikali imetoa fedha nyingi katika wilaya hiyo kwa shughuli za maendeleo.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro leo Septemba 30,2025 akiendelea na mikutano ya kampeni za uchaguzi Mkuu Dk.Samia amesema pia Serikali itaendelea kujenga vituo vya afya vyenye zana kamili za matibabu, dawa na watumishi. “Tutaendelea kufanya kazi hiyo.”
"Kufa kupo lakini kujifungua isiwe sababu. Kwa wilaya ya Same tunakwenda kukamilisha ujenzi wa vituo vitatu vya afya na zahanati tano," amesema na kusisitiza serikali inakwenda kujenga vituo vya afya katika kata za Mdee na Mshewa.
Kwa upande wa maji safi na salama amesema Serikali imeongeza kiwango cha upatikanaji maji kutoka asilimia 45 hadi asilimia 95 katika maeneo ya mjini.
Vilevile kwa vijijini kutoka asilimia 49 hadi asilimia 65 huku akieleza kuhusu kukamilika awamu ya kwanza ya mradi wa Same - Korogwe ambao umeanza kutoa huduma.
"Tunajipanga kwenda na awamu ya pili ambayo tutamalizia kata zilizobaki upande wa Same na kuingia Korogwe," amesema.
Kuhusu barabara amesema Serikali ilianza ujenzi wa barabara ya Mkomazi - Same yenye urefu wa kilometa 101 ambapo imagawanywa vipande viwili."Niwahakikishie tunakwenda kukamilisha barabara hii muhimu kwa usafirishaji mazao ya kilimo.”
Pia amesema anatambua Tarafa ya Mamba kunapolimwa Tangawizi wakati wa mvua ni shida kuteremsha tangawizi kwenda maeneo mengine ,hivyo Serikali inakwenda kuzijenga barabara za milimani kwa kutumia zege na lami," aliongeza.
Awali Katibu Mkuu CCM, Balozi Dk. Asharose Migiro, amesema makubwa yamefanyika katika Mkoa wa Kilimanjaro ambapo ametoa mwito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29 mwaka huu kumpigia kura Dk. Samia.
"Tujue siku hiyo tunapigia kura maendeleo, tunapigia kura uboreshaji miundombinu, tunapigia kura jitihada ambazo zimefanywa na CCM chini ya Uenyekiti wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha afya, maji, mazingira bora ya biashara.
"Hayo ndiyo yatakuwa katika boksi la kura Oktoba 29 mwaka huu. Tujitokeze kwa wingi kuhakikisha tunakipa nguvu CCM, tunampa nguvu mgombea wetu Dk. Samia, wabunge na madiwani ili waendeleze kazi nzuri waliyoianza.”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...