Akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo mwisho wa wiki jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa NBC, Bw Elvis Ndunguru, pamoja na kuwajengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma mbalimbali mpya za benki hiyo alisema ujio wa dawati maalum la wataalam wabobevu kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi utasaidia benki hiyo kuwa karibu zaidi na wadau wa sekta hizo kwa kubuni huduma zinazoendana na mahitaji halisi ya wadau hao.
“Huu ni muendelezo tu wa matukio kama haya, tumekuwa tukitumia fursa kama hizi kujadili na wateja wetu namna tunavyoweza kuboresha huduma zetu kulingana na mahitaji yao. Tukiwa kama muhimuli muhimu wa utoaji wa huduma za kifedha nchini, NBC tunatambua umuhimu wa utoaji wa huduma bora kwa wateja na kukuza ushirikiano kati yetu na wateja wetu. Hii inasababishwa na mabadiliko yanayotokana na ubunifu na maendeleo ya kiteknolojia.’’ Alisema Ndunguru.
Aidha, kupitia mpango huo benki hiyo imekuwa ikielezea mikakati yake mipana inayolenga kuwahudumia kwa ufanisi zaidi wateja hao, kuwajengea mitandao ya kibiashara miongoni mwao sambamba na kuwasogezea huduma za kibenki karibu zaidi huku huduma ya NBC Connect ikitajwa kama suluhisho muhimu katika kuwasogezea huduma za kibenki wateja hao wakubwa yakiwemo mashirika na kampuni binafsi, pamoja na taasisi za serikali.
“Tunaamini kuwa msingi wa huduma za kipekee ni kuelewa mahitaji na matakwa ya wateja wetu, ziara hizi zinatupatia mitazamo au maono yatakayosaidia kuwa wabunifu na kuboresha uzoefu wa kibenki kwa ujumla. Kupitia matukio kama haya tuliweza kugundua mahitaji halisi ya wateja wetu kutoka sekta ya biashara na tukaweza kubuni huduma zinazojibu maswali yao. Sasa tunakwenda kufanya hivyo hivyo kwa wadau wa sekta nyingine muhimu zikiwemo sekta za madini, kilimo na uvuvi ili tuendelee kuja na huduma stahiki kwao ikiwemo mikopo, bima na elimu zaidi kuhusu uendeshaji wa kisasa wa shughuli zinazohusiana na sekta hizo. ” Aliongeza Bw Ndunguru.
Aidha, Bw Ndunguru alitaja baadhi ya mambo muhimu ambayo benki hiyo imekuwa ikiyazingatia katika kukuza ushirikiano na taasisi za kibiashara hapa nchini kuwa ni pamoja na utoaji wa suluhisho zenye ubunifu katika huduma za kifedha, ubunifu wa kiteknolojia, ubia wa kimkakati, kukuza ukuaji wa uchumi pamoja na uwajibikaji kwa jamii huku kipaumbeke kikiwekwa zaidi kwenye masula ya elimu, afya na uhifadhi wa mazingira.
Hafla hiyo pamoja na wateja pia ilihusisha uwepo wa maofisa wengine waandamizi wa benki ya NBC kutoka mikoa tofauti ya Kanda ya ziwa na Makao makuu ya benki hiyo akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki hiyo, Bw Msafiri Shayo.
Wakizungumzia hatua hiyo baadhi ya wateja wa benki hiyo mkoani Mwanza wameipongeza benki ya NBC kwa hatua hiyo muhimu huku wakionesha kuvutiwa zaidi na huduma ya NBC Connect.
“NBC Connect imerahisisha sana maisha yetu hasa kwenye upande wa miamala na namna ya upatikanaji wa huduma za kibenki. Jukwaa hili la kidigital maalumu kwa ajili ya taasisi na biashara kubwa linarahisisha zaidi ufanyaji wa miamala ikiwemo kufanya malipo ndani ya nchi kwa TISS ambapo kwasasa tunaweza pia kufanya malipo ya nje kwa urahisi na usalama zaidi,’ alisema mmoa wa wateja hao Bi Nyanjige Ngambeki kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kauli iliyoungwa mkono na Bw Rajab Kinande, Meneja wa PSSSF Kanda ya Ziwa.
Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw, Elvis Ndunguru (kushoto) akizungumza na wageni waalikwa ambao ni wateja wa benki hiyo jijini Mwanza wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wakubwa kutoka makampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo. Hafla hiyo iliyoandaliwa kupitia timu ya Biashara na Uwekezaji (CIB) ya benki hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Mwanza.
Baadhi ya wateja wa benki ya NBC jijini Mwanza wakifuatilia hafla hiyo
Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw, Elvis Ndunguru (kushoto) akiwaongoza maafisa mbalimbali wa benki hiyo kusalimiana na wateja wa benki hiyo jijini Mwanza wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wakubwa kutoka makampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo. Hafla hiyo iliyoandaliwa kupitia timu ya Biashara na Uwekezaji (CIB) ya benki hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Mwanza
Hafla hiyo pamoja na wateja pia ilihusisha uwepo wa maofisa wengine waandamizi wa benki ya NBC kutoka mikoa tofauti ya Kanda ya ziwa na Makao makuu ya benki hiyo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...