Mwamvua Mwinyi, Mafia, Septemba 25,2025
Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya hiyo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya malisho ya mifugo ili kuepusha migogoro kati ya wafugaji na wakulima.


Ametoa agizo hilo septemba 24,2025 eneo la Kibaoni, Kata ya Kiegeani, wakati wa uhamasishaji wa utoaji wa chanjo kwa mifugo, ambapo wilaya ya Mafia imepokea dozi 49,600 za chanjo ikiwemo dozi 40,000 za kuku, 8,000 za ng’ombe na 1,600 za mbuzi na kondoo.


Chanjo zilizotolewa katika zoezi hilo ni pamoja na homa ya mapafu kwa ng’ombe, sotoka kwa mbuzi na kondoo, na chanjo ya kideri (mdondo), ndui na mafua ya kuku kwa kuku wa kienyeji.


Mangosongo alisema ni muhimu kwa wafugaji na wakulima kuishi kwa amani na mshikamano, akisisitiza kuwa njia bora ya kuzuia migogoro ni kuhakikisha wafugaji wanapatiwa maeneo maalum ya malisho.


“Ni vyema wafugaji waandaliwe maeneo ya malisho ili kuepuka hali ya mifugo kuzagaa mijini na kuingia kwenye mashamba ya watu, tusifanye wafugaji waonekane kama wametelekezwa,” alisema.


Aidha, alitoa onyo kali dhidi ya vitendo vya wizi wa mifugo, akieleza kuwa ni kinyume cha sheria na yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.


Mangosongo alisisitiza ,umuhimu wa wafugaji kuwa na mazizi ya mifugo katika maeneo yao ili kupunguza matukio ya wizi, kuzuia mifugo kuingia mashambani na kudhibiti usambao holela wa mifugo.


Anawataka maofisa ugani kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ipasavyo.


Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Seleman Kataga, aliwataka wafugaji kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la chanjo ili kudhibiti milipuko ya magonjwa na kuongeza uzalishaji wa mifugo na mazao yake kwa ubora unaotakiwa.


Zoezi la chanjo linafanyika kitaifa na linaenda sambamba na utambuzi wa mifugo kwa njia ya kielektroniki huku Serikali ikiwa imetenga kiasi cha sh. bilioni 216 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo inachangia nusu ya gharama ya chanjo hizo.


Hadi sasa, kuku 36,137 wamekwishachanjwa, sawa na asilimia 90 ya lengo la uchanjaji wa kuku, huku zoezi la uchanjaji wa ng’ombe likiendelea ambapo tayari ng’ombe 117 wamechanjwa.


Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...