*Pia imo miradi ya ujenzi wa bandari mbili, barabara na Liganga, Mchuchuma

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Samia Suluhu Hassan amehutubia maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma huku akitumia nafasi hiyo kuelezea mambo makubwa ya maendeleo ambayo yatakwenda kufanyika katika miaka mitano ijayo.

Akihutubia wananchi hao katika Uwanja wa Mbambabay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma leo Septemba 21,2025 Mgombea urais Dk.Samia amesema Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2025-2030 itakwenda kutekeleza mambo ambayo yataleta maendeleo na uimarishaji taifa na kustawisha hali za wananchi.

"Ile ndoto ya muda mrefu ya wananchi wa Nyasa kuwa na bandari ya uhakika inaelekea kutimia mapema mwakani. Lakini vilevile, mtakumbuka nilizindua barabara ya Mbinga - Mbambabay yenye urefu wa kilometa 66 ambayo ni kiunganishi kati ya Bandari ya Mtwara na Bandari ya Mbambabay.

"Tulikamilisha ujenzi wa Bandari ya Ndumbi ambayo tayari imekamilika na inaendelea kufanyakazi. Bandari hii katika kufanyakazi kwake baada ya kujengwa imeongeza uwezo wa kuhudumia shehena kutoka tani 40,000 hadi tani 100,000 kwa mwaka," amesema Dk.Samia.

Ameongeza kwamba abiria waliosafirishwa kupitia bandari hiyo imetoka wastani wa watu 45,000 hadi 100,000 kwa mwaka huku pia akieleza Bandari ya Ndumbi ni ya kimkakati kuhakikisha usafirishaji watu na bidhaa.

Aidha amesema pia Serikali inatekeleza mradi mkubwa ambao tafiti zimeshakamilika wa ujenzi reli yenye urefu wa kilometa 1,000 ambayo itapita maeneo yenye utajiri mkubwa wa nafaka.

Pia amesema itaunganisha maeneo ya kiuchumi ya Liganga na Mchuchuma yenye utajiri mkubwa wa chuma na makaa ya mawe."Tupo kwenye mazungumzo tuweze kujenga reli hii ya kisasa kwa viwango vya kimataifa kutoka Mtwara hadi Mbambabay.

Dk.Samia amesema kwamba “Hayo ndiyo tunayoyafikiria kwa Wilaya ya Nyasa.Ni wazi reli hii tukiweza kuijenga itaambatana na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa ukanda wa kusini.”

Akifafanua Dk.Samia katika Wilaya ya Nyasa kuna miradi mikubwa mitatu ambapo wa kwanza ni bandari zao mbili ,barabara inayounganisha hizo bandari na reli tunayoifikiria kuijenga pamoja na Mchumchuma na Liganga."

Kwa upande wa sekta ya afya amesema katika sekta ya afya maboresho yamefanyika katika hospitali ya wilaya, vituo vitatu vya afya na kujenga kipya kimoja.Serikali imejenga zahanati mpya tisa pamoja na kuajiri watumishi wa afya 316.

Akizungumza kuhusu sekta ya elimu amesema Wilaya ya Nyasa imenufaika kupitia ujenzi wa shule mpya 12 ambazo sita za msingi na sita za sekondari pamoja na chuo cha ufundi stadi.”Lengo la chuo hicho ni kuchochea ajira kupitia ujuzi watakaopata vijana ambao wataanzisha viwanda.”

Kwa upande wa nishati, Dk.Samia kwamba umeme umefikishwa vijiji vyote vya Wilaya ya Nyasa, vitongoji 153 huku bado kazi ya kusambaza nishati hiyo katika vitongoji 423 ikiendelea.

Amesema anafahamu Wilaya ya Nyasa kuna changamoto ya umeme kuwa mdogo, hivyo wamepokea pendekezo na watajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme ambacho kitapokea umeme kutoka Songea, uingie Nyasa kisha usambazwe

"Na hiyo inakwenda kuondoa tatizo la umemw kuwa mdogo na sasa tutavutia wawekezaji kuja Nyasa kwa sababu Bandari Mbili zinafanyakazi, reli tukijaaliwa itakuja, Linganga na Mchuchuma mwekezaji tunamalizana naye aingie.”

Pamoja na hayo amesema serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ikiwemo ujenzi wa Daraja la Mtu Luhuhu linalounganisha Ruvuma na Njombe.

Pia serikali itaendeleza ujenzi wa barabara kuu ya Kidatu - Ifakara - Malinyi - Londo hadi Lumecha yenye urefu wa kilometa 512 ambayo inaunganisha Ruvuma na Morogoro.

"Tayari tumekamilisha kilometa 61 na imani yangu tunakwenda kukamilisha sehemu iliyobakia," amesema Dk.Samia.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...