*Ampongeza kwa uwezo wake wa kutafuta na kusimamia vizuri mgawanyo wa rasilimali fedha 

*Asema heshima ya kumfanya kuwa msaidizi wake ni heshima ya wana Ruvuma wote.

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema katika mikoa 11 ambayo tayari amefanya mikutano ya kampeni wananchi wameshasema kwamba  watampigia kura za kishindo Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama hicho, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29,2025.

Dk.Nchimbi ameyasema hayo leo Septemba 21,2025 alipokuwa akizungumza katika mkutano wa kampeni za Urais uliofanyika Mbambabay katika Wilaya ya Nyasa Mkoa wa  Ruvuma ambapo ametumia nafasi hiyo kumshukuru na kumpongeza Dk. Samia kwa usimamizi mzuri wa rasilimali fedha ambazo zinatumika kuleta miradi ya maendeleo nchini.

Amefafanua katika kuomba  kura alipangiwa maeneo ya kupita kama msadizi wake na mpaka sasa ameshapita  mikoa 11. “Naomba nikupe salamu katika mikoa hiyo 11, imenituma nikuambie kwamba utashinda wewe (Dk. Samia) na CCM kwa kishindo katika mikoa yote 11.

"Wamenituma nikwambie, wabunge wa CCM watashinda kwa kishindo, madiwani wa CCM watashinda kwa kishindo na Rais wao kipenzi Dk. Samia Suluhu Hassan atashinda kwa kishindo," amesema.

Aidha amemshukuru  Rais Dk. Samia kwa kumpendekeza kuwa mgombea mwenza wa Urais ambapo aliahidi kumsaidia kiongozi huyo kwa uaminifu."Heshima hii siyo yangu pekee ni heshima kwa Mkoa wote wa Ruvuma, tunakushukuru sana. 

“Nikuhakikishie kwa mila zetu Mkoa wa Ruvuma imani huzaa imani, nitakusaidia kwa uwezo wangu wote kwa uaminifu wangu wote kuhakikisha unatekeleza ilani ya CCM kama ulivyokusudia. Pia unafikia maono yako ya kulikomboa taifa letu kutoka hali duni kuwa hali bora Zaidi.”

Dk.Nchimbi pia amesema atakuwa msaidizi  mwaminifu na kwa nguvu zangu zote huku akieleza kwa niaba ya wana Ruvuma wanamshukuru kwa maendeleo makubwa aliyoyafanya na  siyo kwa Ruvuma tu bali Tanzania nzima.

“Uwezo  wako wa kutafuta rasilimali, uwezo wako wa kusimamia mgawanyiko wake kuhakiksha kila pembe ya nchi yetu inapata rasilimali bila ubaguzi.Umetufanya CCM tusimame kifua mbele kukinadi chama chetu, uwezo wako umetupa heshima ya kuaminiwa na Watanzania ambapo kila kona tunapata ahadi za kishindo. 

“WanaCCM wote, wananchi wote wa Mkoa wa Ruvuma tutahakikisha  tunapiga kura za heshima kwa Rais wetu ambazo zitampatia nguvu kuendelea kututumikia ambazo zitawaonyesha dunia nzima kwamba tunaimani na mapenzi kwa Rais."
















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...