*Aelezea pia umeme wa uhakika, kuvutia wawekezaji wa viwanda

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Kigoma

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Kigoma Serikali itahakikisha miradi yote ya barabara inayoendelea katika Mkoa wa Kigoma inakamilika ikiwemo vipande vyote vilivyosalia vya barabara kuu.

Baadhi ya vipande hivyo vya barabara ni kutoka Manyovu hadi mpakani pamoja na barabara zote zilizoahidiwa mkoani humo katika mikutano yake ya kampeni.

Akizungumza leo Septemba 14,2025 mbele ya maelfu ya wananchi wa Jimbo la Kigoma Mjini katika uwanja wa Katosho ,Mgombea urais Dk.Samia amesema ahadi nyingine ni kuhakikisha barabara za vijijini ambazo hazipo katika mpango wa kuwekewa lami, zinajengwa kwa changarawe kuzifanya zipitike misimu yote.

Akizungumzia umeme,Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inatekeleza mradi wa Mto Malagalasi ambao utazalisha megawati za umeme 49.5 kisha kujengwa msongo wa kilovoti 132 kutoka Malagalasi hadi Kidahwe wenye urefu wa kilometa 54.

Ameongeza umeme huo utafikishwa katika kituo cha kupoza nishati hiyo kilichopo Kidahwe kisha kusambazwa katika maeneo mengine ya mkoa huo huku akifafanua miundombinu ya umeme katika mkoa huo imefikishwa kwenye vijiji vyote na sasa Serikali inamaliza kusambaza nishati hiyo katika vitongoji.

Pia, amesema uwepo umeme kutosha ndani ya mkoa huo utajenga mazingira rafiki kuvutia uwekezaji akitolea mfano uwekezaji mkubwa uliofanyika wilayani Kasulu wa kiwanda cha sukari ambacho kimeajiri watu 500.

Ameongeza kitakapoanza kufanyakazi kwa ukamilifu, kitaongeza upatikanaji sukari nchini hivyo kuleta utulivu wa bei kwa ajili ya walaji.

Dk. Samia amesema katika mkoa huo pia kuna kiwanda kikibwa cha saruji ambacho kinazalisha bidhaa hiyo kwenye soko la Kigoma na nchi Jirani.

Akieleza zaidi Dk.Samia amesema katika miaka miaka mitano ijayo wakipata ridhaa Serikali inayo mpango wa kuvutia viwanda vingi kuja ndani ya Kigoma na hatutasahau suala la kongani za viwanda kwa vijana kuongeza thamani mazao yanayozalishwa hapa. Taifa letu tumejipanga kuhakikisha tunajitosheleza uzalishaji mafuta ya kupikia.

"Michikichi ni sehemu muhimu ya mpango huo, ninafahamu bado kuna eneo la kulima chikichi ambalo ni kubwa lakini bado halijafanyiwa kazi, vilevile uhitaji wa miche milioni moja bado hatujalifanyiakazi.

“Niwatake ndugu zangu wakulima wa chikichi serikali mkitupa ridhaa tunakwenda kujielekeza kwenye kilimo cha michikichi kwa nguvu kubwa ili tupate malighafi nyingi tuweze kuvutia kiwanda cha kuchakata chikichi na kutengeneza mafuta nchini.

"Tunapokuwa na mpango huo, tutatoa ruzuku ya miche na mambo mengine yanayohitajika ili chikichi zilimwe kwa wingi tuweze kuvutia viwanda. Serikali ya CCM ina mkakati wa kuona wawekezaji wengi wanaendelea kuja Kigoma, miongoni mwa ahadi zetu ni kongani za viwanda. Uzuri hapa Kigoma soko lipo Jirani na ni soko kubwa.”

Dk.Samia amesema pia kila kinachozalishwa Kigoma kikivuka kwenda Burundi na DRC hayo ni masoko makubwa sana na wala hatuwezi kukamilisha mahitaji yao.”Niwaombe tujielekeze huko."

Kuhusu sekta ya afya, elimu, umeme na maji amesema uwekezaji mkubwa umefanyika, hivyo ahadi ya Chama chake ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma safi za afya, elimu na kupeleka umeme katika vitongoji vyote.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...