*Aainisha utekelezaji wa Ilani iliyopita, aanika yanayokwenda kufanyika miaka mitano ijayo

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Tabora

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema ameona maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika mkoa ambayo imetekelezwa katika miaka mitano iliyopita na iwapo watapata ridhaa ya wananchi Serikali itafanya makubwa zaidi katika miaka mitano ijayo.

Akizungumza katika mkutano uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi na Wana CCM wa Mkoa wa Tabora leo Septemba 12,2025 Mgombea Urais Dk.Samia Suluhu Hassan ameeleza maeneo yote ya mkoa huo ambako amepita amejionea maendeleo makubwa yaliyofikiwa.

"Jana nilikuwa Wilaya ya  Kaliua .Mwaka 2023 nilikuja katika ziara ya kikazi lakini  nimeingia Kaliua jana siyo ile kuna mabadiliko na maendeleo makubwa sana. Lakini pia maeneo yote nikipita maendeleo yanaonekana kwa macho tena kwenye sekta zote," 

Dk.Samia ameeleza kuwa katika sekta ya afya, elimu, maji, nishati na kilimo mambo makubwa yamefanyika huku akifafanua Serikali inafahamu bado maendeleo hayo hayajatosheleza kwa  sababu wananchi wanaendelea kuongezeka.

"Watu wanazaliwa wanakuwa wakubwa  hivyo tunajua madarasa yatahitajika, vituo vya afya na matibabu yatatakiwa kila siku, maji yatahitajika, nishati utatakiwa kila siku kwa sababu maendeleo ya viwanda na mengine yanayohitaji umeme yanaendelea kukuwa ndani ya nchi yetu.

“Hivyo, Serikali ya CCM itakapopata ridhaa itasogeza karibu maji, umeme, kilimo na ufugaji. Hata shughuli za uvuvi nazo zitajumuishwa.Serikali itaendelea kwenda kufanya shughuli za maendeleo kwa nguvu kubwa zaidi kama ilivyofanya miaka mitano iliyopita.

Aidha Dk.Samia amesema katika wilaya za Urambo na Kaliua, umeme ulikuwa  hautoshelezi mahitaji ambapo serikali iliahidi kujenga kituo cha kupoza umeme na sasa tatizo hilo limemalizika.

“Serikali itajenga kituo cha kudhibiti mifumo ya usambazaji umeme eneo la Ziba wilayani Igunga ili kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji itakapokamilika, vituo hivyo vitadhibiti, kupoza na kusambaza nishati hiyo.

“Serikali  iliahidi kufanya upanuzi na ukarabati kiwanja cha ndege Tabora kazi ambayo imefikia asilimia 95 huku kiwanja kikiendelea kutumika. Tabora tunakwenda kuwa na kiwanja kikubwa na kizuri cha kutua ndege kubwa zaidi," amesema.

Kuhusu sekta ya kilimo, amesema Serikali  inakwenda kuweka mkazo kutoa ruzuku kwa wakulima kuanzia mbolea, pembejeo na chanjo.Pia Serikali itakwenda kufanya maboresho ya minada, ujenzi wa majosho na kutoa zaidi chanjo ya mifugo.

Mgombea urais Dk.Samia amesema kuhusu upande wa kilimo cha mazao, amesema
Serikali inakwenda kuendelea na ujenzi na ukarabati wa skimu za kumwagilia ili wakulima waweze kuzalisha mara mbili kwa mwaka.

"Kuna miradi inayoendelea kutekelezwa itakapokamilika tunatarajia Mkoa wa Tabora uwe na maji ya kutosha. Na kila mwananchi apate maji ya kutosha," alisisitiza.

Amesema  kupitia mradi unaotoa maji Ziwa Victoria na ule wa miji 28 utakwenda kuondoa changamoto ya maji ndani ya mkoa huo huku akikisitiza ipo miradi ya kitaifa ambayo inapita mkoani Tabora.

Dk.Samia ameitaja baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga.“Mradi huo unapita katika wilaya za Nzega na Igunga, unakwenda kuzalisha ajira kwa vijana watakaokuwa na sifa za kufanyakazi katika mradi huo.”

Vilevile, amesema ujenzi wa reli ya mwendokasi (SGR) ambao unatoka Makutupora kuja Tabora na Tabora kwenda Isaka, utafungua fursa zaidi.Mradi mradi huo unapita katika wilaya za Uyui, Urambo na Kaliua ambapo vitajengwa vituo vya kushusha na kupakia abiria.

"Katika maeneo ya vituo maendeleo mbalimbali yatakuja, biashara zitakazowekwa kupitia sekta binafsi lakini pia maghala ya kuhifadhi bidhaa zitakazosafirishwa na reli hiyo.

"Hiyo ni ajira na fursa za biashara ambazo tungeomba wananchi wa Tabora wazitumie ili kukuza uchumi, kupata ajira na kuendeleza biashara.”



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...