Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Tabora

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha  Mapinduzi(CCM) Dk.Samia Suluhu Hassan amehutubia maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora huku akitumia nafasi hiyo kuelezea mipango ya Serikali katika miaka mitano ijayo.

Akizungumza leo Septemba 11,2025 katika mkutano uliofanyika katika Kata ya Ilolanghulu wilayani Uyui mkoani Tabora, Dk.Samia Suluhu Hassan amesema wananchi wa wilaya hiyo waliomba watumishi katika sekta ya elimu na tayari walishachukua hatua kwa kuajiri walimu.

"Ninafurahi kuwaambia leo kwamba tumeajiri walimu 412 ambao wameletwa ndani ya Wilaya hii ya Uyui.Lakini na watumishi wa afya 161.Tunapoendelea mbele najua bado mahitaji ya watumishi yapo.

"Niliahidi ndani ya siku 100 mtakaponipa ridhaa kuendelea kuongoza nchi hii. Ndani ya siku 100 tutaajiri kwenye sekta ya afya watumishi 5000 bila shaka wengine watafika na Uyui.”

Mgombea Urais Dk.Samia pia amesema kwamba  katika siku hizo 100 serikali yake itaajiri watumishi 7000 ambapo wilaya hiyo itanufaika.

“Katika  sekta ya afya ndani ya wilaya hii Serikali  imeleta Sh.bilioni 8.2 ambazo zimetumika kujenga vituo vya afya na kuboresha hospitali ya wilaya,”amesema na kuongea pia fedha hizo zimetumika kujenga vituo vya afya sita na zahanati mpya 17.

Pia amesema katika Wilaya ya Uyui amesema kuwa Serikali ilishapeleka  magari matatu ya kuhudumia wagonjwa ambayo yanaendelea kufanyakazi kuhudumia wananchi.

"Nafahamu wilaya ni kubwa, hivyo mahitaji ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati bado yapo. Tumejielekeza kusaidia pale ambapo nguvu za wananchi zimeanza na serikali itakuja kumalizia," alieleza.

Akizungumzia sekta ya elimu, amesema kwamba Serikali imeongeza shule saba za sekondari hivyo kufikia 34 kutoka 27 za awali huku akifafanua idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 12,000 hadi 17,500.

“Serikali imeongeza shule za msingi 28 kutoka 124 hadi 182 na kuendelea kutoa elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.

"Tumejenga madarasa ya chekechea. Hii ni programu maalim ya mwendeleo wa mtoto mapema, tunaweka madarasa haya kwa sababu mama na baba zao hawakuanza shule mapema.

Aliongeza: "Walianza kwenda kwenye ng'ombe kwenye shamba lakini sasa tumeanzisha programu ya kumwezesha mtoto aanze shule mapema."

Alieleza kuwa hiyo ndiyo sababu kwa shule mpya zinazojengwa nchini yanajengwa madarasa ya chekechea ili watoto waanze kukuza akili zao mapema.

Kadhalika, alisema serikali imetekeleza programu za kuimarisha sekta za kilimo na mifugo.

"Tumejenga skimu za umwagiliaji zikiwemo Goweko na Unyanyama na kuendelea kutoa ruzuku ya mbolea, mbegu na dawa za chanjo kwa wafugaji.

"Tunapoendelea mbele tutaendelea na ujenzi wa majosho na mabwawa kwa ajili ya mifugo," alibainisha.

Kwa upande wa sekta ya maji Mgombea Urais Dk.Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa katika wilaya hiyo kulikuwa na miradi 15 ambayo imeongeza upatikanaji maji hadi asilimia 67.

“Hata hivyo  bado kuna baadhi ya maeneo ambayo hayajapata maji, lakini kupitia mradi wa Ziwa Viktoria serikali itajenga tanki kubwa la lita milioni moja katika Kata ya Ilolanghulu.Ujenzi wa tanki hilo litahudumia wananchi wa Ilolanghulu pamoja na kata za Kalola, Isila, Ndono na Mabana.

Aidha Dk.Samia amesema  ipo miradi ya maji Kigwa, Kizengi na bwawa la Igombe ambayo imefikia hatua mbalimbali za utekelezaji wake.

"Ahadi yangu kwenu ni kuimarisha miradi hiyo ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maji safi na salama.Mwaka 2022 nilipokuwa hapa mlinieleza kuhusu uhitaji wa daraja la Mto Roya, sasa nataka niwajulishe tumekamilisha usanifu, michoro na gharama ya daraja hilo.

Alisisitiza: "Tumeshatenga fedha ndani ya mwaka huu wa fedha kwa hiyo tunatafuta mkandarasi ili daraja lianze kujengwa. Tutakapojenga tutasaidia wananchi kuvuka kwa raha wakati wa masika."

Kuhusu madeni ya wakulima wa tumbaku, Dk.Samia ameanza kwa kuwapongeza kwa kuongeza uzalishaji wa zao hilo huku akieleza kupitia mbolea na pembejeo za ruzuku wameongeza uzalishaji wa tumbaku.Hivyo kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazouza tumbaku nyingi duniani.

Hata hivyo amewakikishia wakulima  serikali bado ipo katika mazungumzo na kampuni za PCL na Volecel ambazo hazijalipa fedha za wakulima.

"Niwahakikishie zitalipwa, kupitia Waziri wa Kilimo huwa ninataka ripoti kila baada ya muda aniambie mazungumzo yamefikia wapi ili wakulima walipwe fedha zao.

Alisisitiza: "Lakini ninafurahi kusema tumeongeza kampuni za kununua tumbaku, sasa kuna ushindani na lile suala la mikopo na wakulima kuchelewa kulipwa fedha zao halipotena."











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...