# Sekta ya uvuvi nayo yaguswa.
Mwanza.
Ujenzi wa Barabara ya Buhongwa-Igoma yenye urefu wa Km 14 kwa kiwango cha lami inayojengwa katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza inatajwa kuwa ndio mwarobaini wa changamoto ya msongamano wa magari jijini humo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Wakili Kiomoni Kibamba wakati akielezea hali ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Jiji la Mwanza kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji na Majiji Tanzania (TACTIC) na manufaa yake kwa wananchi.
Amesema barabara hiyo inayounganisha Kata nne ambazo ni Buhongwa, Lwanhima, Kishiri na Igoma ilikuwa na changamoto kubwa hali iliyopelekea magari yote yaliyokuwa yakitoka Buhongwa kwenda Igoma au Igoma kwenda Buhongwa kulazimika kuingia katikati ya jiji hivyo kuongeza msongamano wa magari.
Wakili Kibamba ameongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utasaidia kupunguza msongamano huo kwa kiasi kikubwa kwani magari yote yaliyokuwa yanatoka maeneo hayo hayatolazimika kuingia katikati ya Jiji badala yake yatakwenda moja kwa moja ama Igoma au Buhongwa.
Vilevile, Mradi wa (TACTIC) katika Jiji la Mwanza unatekeleza Mradi wa ujenzi wa Soko la samaki wabichi Kata ya Mkuyuni ambapo kwa mujibu wa Wakili Kibamba amesema kuwa hiyo ilikuwa ni changamoto iliyokuwa inawakabili kwa muda mrefu.
"Halmashauri ya Jiji la Mwanza tulikuwa na changamoto ya kukosekana kwa eneo la kuuzia mazao ya uvuvi. Ujenzi wa soko la samaki la Mkuyuni litawezesha kunyanyua uchumi kwa sababu hata haya maboti ya uvuvi yanayotoka Wilaya ya Ukerewe na upande wa Buchosa Wilayani Sengerema yatakuwa yanakuja kuuzia samaki kwenye soko hili, kwa hiyo tutafungua uchumi sio wa hapa tu lakini pia imesaidia mazingira ya uwezeshaji wa kufanya biashara kati ya Mwanza na Mikoa mingine" amebainisha Wakili Kibamba
Kwa mujibu wa Wakili Kibamba miradi yote miwili kwa pamoja sio tu imesaidia kulifanya jiji la Mwanza kupendeza lakini imepandisha thamani ya ardhi kwa wananchi sambamba na kurahisisha shughuli za usafirishaji wa watu na bidhaa kwenye maeneo ya miradi.
Kwa upande wake Bw. Kalumanzila Idd, Mkazi wa Buhongwa, jijini Mwanza ameishukuru serikali kwa kuwajengea barabara hiyo kwani imewaondolea adha ya usafiri iliyokuwa inawakabili kwa muda mrefu.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...