
Na Nihifadhi Abdulla, Zanzibar
KATIBU Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Abeida Rashid Abdallah amesema Mpango Jumuishi wa Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto wa Miaka Mitano (5) utakapokamilika utakuwa nyenzo muhimu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Watoto na Malengo ya Kitaifa na Kimataifa.
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu 01-3/09/2025 cha kuandaa Mpango huo kilichofanyaka katika Hotel ya Visitors Inn, Jambiani, Mjini Unguja kilicho andaliwa na Taasisi ya Afisi ya Rais Ufuatiliaji wa Utendaji Serikalini Zanzibar (ZPDB).
Amesema Mpango Jumuishi wa Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto wa Miaka Mitano unahimiza huduma za afya, chanjo, lishe bora na ulinzi wa mtoto na malezi yenye mwitikio, hivyo kuchangia moja kwa moja kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs),hususan lengo nambari nne (4) linalohusiana na Kupunguza Vifo vya Watoto chini ya Umri wa miaka mitano.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi na mikakati yake ya maendeleo, imeweka kipaumbele kikubwa katika masuala ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECD) ili kuhakilisha kila mtoto wa Kizanzibari anapata malezi bora ili aweze kufikia utimilifu wake (potential).
“Programu hii ni muhimu sana kwa kuwa unajikita katika kuhakikisha kila mtoto wa Kizanzibari anapata malezi bora, afya njema, lishe inayostahiki, ulinzi, na fursa ya kujifunza katika hatua za awali za maisha yake” Amesema Abeida.
Akizungumza katika kikao kazi hicho, Mtalaam wa Hifadhi ya Mtoto kutoka UNICEF ndugu Ahmed Rashid Ali amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuekeza katika Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwani faida yake ni sawa na kuwekeza shilingi moja katika biashara na kupata faida ya shilingi saba.
Amesema utafiti umeonesha asilimia 18 watoto wameduma huku asilimia 40 hawakufikia viwango vya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali, hivyo Shirika la UNICEF linafanyakazi ya kushirikina na Serikali ya Mapinzudi Zanzibar kupata kinga na matibabu ya changamoto iliyopo.
Mapema akizungumza, Mratibu wa Programu ya Malezi, Makuzi na maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka ZPDB) Dkt. Maryam Issa amesema lengo la Programu hiyo ni kuhakikisha watoto 276,000 wa Zanzibar wanakua katika mwelekeo unaofaa kwa kuhakikisha wanapata huduma za afya, lishe, ulinzi na usalama wa mtoto ifikapo 2030.
Amesema shughuli mbali mbali zimekuwa zikitekelezwa kupitia program hiyo ikiwemo kufanya utafiti wa hali ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto ya Zanzibar (ECD base line survey), ambapo miongoni mwa matokeo ya utafiti huo yameonesha kwamba Takribani asilimia 32 ya watoto wenye umri wa miaka 0–3 Zanzibar wamechelewa kimaendeleo.
Pia Dkt Maryam amesema Programu hiyo imefanya utafiti mdogo wa kuangalia huduma rafiki za Malezi na makuzi ya mtoto katika masoko, hospitali na skuli za maandaalizi kwa Unguja na Pemba. hali ambayo inaonesha kuwa huduma hizo hazipo, hivyo programu inakwenda kuweka huduma hizo katika maeneo niliyoyataja.
Aidha amesema Maandalizi ya Mtaala wa Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii yamekamilika. Na sasa tayari mafunzo kwa wahudumu hao wa afya yameanza katika maeneo ya Unguja na hatua inayofata wanatarajia Kwenda kisiwani Pemba kutekeleza.
Naye Afisa Muandamizi kutoka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji Maliasili na Mifugo amesema Wizara hiyo inazalisha asilimia 60 ya vyakula vya mboga mboga, protini, vitamini lakini shida iliyopo ni katika uelewa wa mlaji kwani tatizo lipo kwa wenye watu wenye uwezo na wasiokuwa na uwezo hivyo elimu ya lishe inahitajika kwa jamii.
Programu ya ECD inaratibiwa na Afisi ya Rais Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (ZPDB) na inatekelezwa kwa mashirikiano kati ya Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya Kilimo Umwagiliaji,Maliasili na Mifugo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...