Septemba 10, 2025

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameziagiza wilaya na halmashauri mkoani humo kuhakikisha zinadhibiti  matumizi batili ya fedha za mpango wa lishe na badala yake zitumike kwa matumizi yaliyokusudiwa.

Aidha, amezitaka mamlaka hizo kutoa fedha hizo kwa wakati na kwa kiasi kilichopangwa, bila ucheleweshaji wowote.

Akifunga kikao cha lishe cha mkoa wa Pwani kilichofanyika Septemba 9, 2025, Kunenge alieleza kuwa baadhi ya halmashauri zimekuwa zikitumia fedha hizo kwa shughuli tofauti, jambo ambalo ni kinyume na miongozo ya matumizi ya rasilimali hizo.

“Kwa kufanya hivyo, hamtendi haki. Fedha hizi zinalenga kusaidia jamii, hususan watoto, Huwezi kuwa na Taifa linaloendelea kama wananchi wake hawana afya njema wala lishe bora," alisema Kunenge.

Aliwataka wataalamu na watendaji wa sekta husika kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ili kuona jinsi masuala ya lishe yanavyopewa kipaumbele na kuhakikisha yanaingizwa katika mipango ya utekelezaji kwenye ngazi zote.

“Tuweke lishe kama ajenda ya msingi. Hakikisheni Mkoa wa Pwani unaendelea kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika utekelezaji wa afua za lishe,” alisisitiza.

Aidha, Kunenge aliwataka wananchi kuendelea kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara, ili kujitambua kiafya na kuchukua hatua stahiki mapema.

Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, alisema moja ya maeneo muhimu ya kuzingatia ni kuhakikisha afua za lishe zinatengenezwa kwa kuzingatia hali halisi ya jamii, na kuchangia katika uimarishaji wa afya bora.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...