Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ally Ussi (wa tatu kushoto) akizindua tawi la Nyakatuntu wilayani Kyerwa. Pamoja naye ni Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mheshimiwa Zaitun Abdalla Msofe (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Wateja wa Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul (wa nne) pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki ya CRDB, Joseline Kamuhanda.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ally Ussi (wa pili kushoto) akifungua pazia kuzindua tawi la Benki ya CRDB Nyakatuntu akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Wateja wa Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul (wa pili kulia), Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mheshimiwa Zaitun Abdalla Msofe (wa kwanza kulia), na Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta (wa kwanza kushoto).
======== =========
Kyerwa. Tarehe 11 Septemba 2025: Akizindua tawi la Benki ya CRDB Nyakatuntu wilayani hapa, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ally Ussi, ameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kufikisha huduma kwa Watanzania waliopo ndani na nje ya nchi akitolea mfano ofisi yake ya Dubai.
Ussi amesema Tanzania ya sasa imepiga hatua kubwa ya maendeleo hivyo wananchi wake wanahitaji huduma bora za benki ili kufanikisha malengo yao ya kibiashara na uwekezaji, mambo yanayowasaidia kuondokana na umasikini.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu hii ya sita chini ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwa kiasi kikubwa. Sasa hivi Watanzania wanafanya biashara kuanzia vijijini mpaka mjini. Na zaidi wapo wanaoenda nje ya nchi hasa China, Uturuki na kwingineko. Nawapongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zenu za kuwafuata wananchi. Sio tawi hili la Nyakatuntu pekee, mpango wenu wa kufungua ofisi Dubai utaitangaza nchi yetu pamoja na kuongeza kujiamini kwa wananchi wetu pindi wanapokuwa nje ya nchi yetu,” amesema Ussi.
Kiongozi huyo amesema ni wakati sasa wa Watanzania kuanza kuzitumia vyema fursa za uwekezaji zilizopo nchini kwa kushirikiana na taasisi imara za fedha hasa Benki ya CRDB yenye uwezo wa kuwahudumia wakiwa ndani ya nchi na nje ya mipaka yetu kwa viwango vilevile.
“Tunazunguka Tanzania nzima, naomba niwaambie ukweli wana Nyakatuntu, kila tulipopita, katika halmashauri zote, tumekuta kuna mawakala na tawi la Benki ya CRDB. Uzuri wa benki hii ni kwamba ina matawi mpaka nje ya nchi. Ukiwa hapa Kyerwa hauna wasiwasi kufanya biashara na mtu aliyepo Burundi kwa sababu Benki ya CRDB ipo kule. Malipo yako utayapata kwa urahisi kabisa. Litumieni tawi hili kuimarisha biashara zenu na kukamilisha mipango mingine ya kiuchumi,” amesisitiza Ussi.
Kabla ya kumkaribisha kiongozi huyo wa mbio za mwenge kitaifa, Mkurugenzi wa Wateja wa Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul amesema tawi la Kyerwa linaifanya Benki ya CRDB kufikisha zaidi ya matawi 260 hivyo kuwa benki yenye mtandao mpana zaidi wa matawi nchini kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania.
“Tawi hili lililozinduliwa leo hapa Nyakatuntu litarahisisha upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi na wakazi wa hapa Nyakatuntu, Wilaya ya Kyerwa, Mkoa mzima wa Kagera na Taifa zima kwa ujumla hata wageni kutoka nje ya mipaka yetu kwani mkoa huu unapokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi. tutaendelea kujenga matawi mapya kila mahali panapostahili ili kuwahudumia wateja wetu kwa haraka,” amesema Bonaventura.
Licha ya matawi, Bonaventura amesema Benki ya CRDB imewekeza kwenye ubunifu unaowapa wateja wake majukwaa tofauti ya huduma unaojumuisha CRDB Wakala zaidi ya 35,000 nchi nzima ambao kwa Mkoa wa Kagera wapo 1,173 wakiwamo 93 wanaotoa huduma katika Wilaya hii ya Kyerwa.
Bonaventura pia alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wana Nyakatuntu kulitembelea tawi hilo kwa ajili ya kupata ushauri wa uwekezaji na fursa nyingine akiwaeleza kuwa sasa hivi Benki ya CRDB inauza hatifungani yake CRDB Al Barakah Sukuk inayofuata misingi ya sharia ingawa inawakaribisha hata wale wasio waumini wa dini ya Kiislamu.
“Mwekezaji wa hatifungani hii atapata faida ya asilimia 12 kwa mwaka. Uwekezaji wake unaweza kufanywa kwa shilingi za Tanzania au dola za Marekani. Kwa shilingi, mtu au taasisi inaweza kuwekeza kuanzia 500,000 na dola ni kuanzia 1,000,” ameeleza Bonaventura.
Mwisho, mkurugenzi amewakaribisha wakazi wa Kyerwa kushiriki semina za ujasiriamali zinazotolewa na CRDB Bank Foundation yakilenga kuwapa wananchi elimu ya fedha, uunganishaji wajasiriamali na masoko mbalimbali na utoaji wa mitaji wezeshi kwa wanawake, vijana na makundi maalumu.
“Tunayafanya haya yote kupitia programu yetu maarufu ya Imbeju ambayo mpaka sasa imshatoa mitaji wezeshi zaidi ya shilingi bilioni 23,” amesema Bonaventura.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...