Katika kuadhimisha Siku ya Usafiri wa Majini Duniani, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limewataka wananchi kupunguza uchafuzi wa plastiki katika bahari ili kulinda rasilimali hiyo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), kila mwaka kati ya tani milioni 19 hadi 20 za plastiki hutupwa baharini, mito na maziwa, huku zaidi ya asilimia 85 ya taka zinazookotwa zikiwa plastiki.

Inaelezwa zaidi ya tani milioni nane za plastiki hutupwa baharini kila mwaka duniani kote.

Akitoa taarifa leo Septemba 26, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum, amesema maadhimisho ya mwaka huu ni fursa ya kutafakari mchango wa sekta ya bahari katika kuunganisha dunia na kukuza biashara ya kimataifa.

“Katika miongo ya hivi karibuni, shughuli za binadamu zimeathiri kwa kiwango kikubwa uwezo wa bahari kutekeleza majukumu yake. Uchafuzi wa plastiki, kemikali za kilimo na viwanda, kumwagika mafuta, uvuvi wa kupita kiasi, uchimbaji wa madini baharini na uchafuzi wa hewa vimeleta athari kubwa kwa bioanuwai ya majini,” amesema Salum.

Ameongeza kuwa uzalishaji wa hewa ya ukaa (CO₂) unasababisha asidi baharini, hali inayoongeza athari kwa viumbe vya majini na kuchochea ongezeko la joto duniani, jambo linalosababisha kupanda kwa viwango vya maji ya bahari na kutishia maisha ya jamii za visiwa vidogo.

Kwa mujibu wa TASAC, kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Bahari yetu, wajibu wetu, fursa yetu”, ikikumbusha jamii umuhimu wa bahari katika kuhifadhi na kusaidia uhai wa viumbe na bioanuwai ya majini.
Ripoti zinaonyesha changamoto kubwa

Pamoja na kuwepo kwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inayoweka wazi wajibu wa kudhibiti taka, ripoti ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inaonesha Tanzania huzalisha hadi tani milioni 20 za taka kila mwaka.

Mtaalamu wa mazingira, Dk. Aidan Msafiri, amesema usalama wa usafiri wa majini pia unahitaji kuzingatia viwango vya Shirika la Bahari Duniani (IMO) vinavyotaka meli kuwa na vifaa vya kisasa vya mawasiliano na uokoaji pamoja na mabaharia kupatiwa mafunzo ya kutosha.

“Ushirikiano wa mataifa, uwekezaji katika teknolojia ya satelaiti na utekelezaji wa sheria kwa ukamilifu ni nguzo muhimu za kulinda maisha ya wasafiri na mali baharini,” alisema Dk. Msafiri.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...