MASHINDANO ya Lina PG Tour msimu wa nne yameanza kutimua vumbi katika viwanja vya Gymkhana mkoani Morogoro yakilenga kuendeleza urithi wa marehemu Lina Nkya, nyota wa zamani wa timu ya Taifa ya wanawake katika mchezo wa gofu.

Mashindano haya yaliyoanzishwa mwaka 2024 na familia ya Said Nkya yamekuwa sehemu ya kumuenzi Lina, aliyefahamika kwa mapenzi yake makubwa kwa gofu na jitihada za kuukuza mchezo huo nchini.

Akizungumza jana, Septemba 25, 2025 Kiongozi wa mashindano, Ayne Magombe alisema michuano hiyo itafanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 25 hadi 28, ikihusisha mashimo 72 na kushirikisha jumla ya wachezaji 137 wakiwemo 65 wa kulipwa na chipukizi, huku wengine 72 wakiwa wasindikizaji.

“Familia ya Lina imeendelea kuyadhamini mashindano haya kwa lengo la kuenzi mchango wake, na sasa tuna mashindano matano kwa mwaka. Tukipata sapoti zaidi kutoka kwa wadau, tunaweza kuongeza mashindano mengi zaidi ili kukuza huu mchezo,” alisema Magombe.

Wachezaji chipukizi kama Prosper Emmanuel kutoka Klabu ya Lugalo na wazoefu wa kulipwa akiwemo Fadhil Nkya kutoka Gymkhana Dar es Salaam, wamepongeza familia ya Lina kwa kuendeleza mashindano hayo wakisema yamekuwa kichocheo kikubwa cha kukuza vipaji na kuongeza ushindani wa kitaifa na kimataifa.

Kwa mujibu wa Fadhil Nkya, mashindano ya Lina PG Tour yamekuwa fursa ya vijana kujiandaa kwa michuano ya kimataifa na yanapaswa kuungwa mkono zaidi na jamii.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...