Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, ikionya kuwa mvua zinatarajiwa kuwa za Wastani hadi Chini ya Wastani katika maeneo mengi ya nchi, huku baadhi ya maeneo machache yakitarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa (IPCC), ametoa taarifa hiyo leo Septemba 11, 2025 wakati akitangaza utabiri huo kwa waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa Ubungo Plaza.

“Vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko usioridhisha wa mvua vinatarajiwa kutawala hasa katika pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki,” amesema Dkt. Chang’a.

Dkt. Chang’a amesema mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara na kaskazini mwa Kigoma, kabla ya kusambaa katika maeneo ya Simiyu na Shinyanga mwishoni mwa mwezi huo. Pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki zinatarajiwa kuanza kupata mvua wiki ya kwanza na ya pili ya Novemba. Msimu huu wa mvua unatarajiwa kuisha Januari 2026.

Aidha, vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajiwa kuambatana na msimu huu, huku maeneo mengi yakikabiliwa na vipindi virefu vya ukavu na usambazaji wa mvua usioridhisha.

Amesema atharii mbali mbali zinaweza kujitokeza katika kipindi hicho ambapo katika kilimo kunatarajiwa kuwa na upungufu wa unyevunyevu katika udongo unaoweza kuathiri ukuaji wa mazao na kusababisha upungufu wa mavuno. Pia, magonjwa na wadudu waharibifu kama mchwa na panya wanaweza kuongezeka.

Katika sekta ya Maji na Nishati Dkt. Chang’a amesema, Kupungua kwa kina cha maji katika mito na mabwawa kunatarajiwa kuathiri upatikanaji wa maji safi na hata uzalishaji wa umeme.

"Jamii inaweza kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama, huku hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayosababishwa na mbu ikitarajiwa kuongezeka." Amesema.

Ameongeza kuwqla, Wafugaji wanaweza kukabiliwa na upungufu wa maji na malisho, hali inayoweza kusababisha migogoro ya ardhi huku pia baadhi ya maeneo yatakayopata mvua nyingi yanaweza kukumbwa na uharibifu wa barabara, mafuriko na kucheleweshwa kwa safari.

TMA imeendelea kuwashauri wakulima kuandaa mashamba kwa wakati na kutumia mbinu bora za kilimo ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza. Wafugaji wametakiwa kupanga matumizi bora ya malisho na maji, huku sekta za usafirishaji, afya, na mamlaka za serikali za mitaa zikihimizwa kuimarisha miundombinu na kuchukua tahadhari za mapema.

Aidha, amebainisha kuwa TMA inaendelea kutoa utabiri wa msimu kwa ngazi ya wilaya. “Wilaya 86 zilizopo kwenye ukanda wa mvua mbili kwa mwaka, zitapatiwa utabiri wa kina wa maeneo madogo,” alisema.

Vilevile, wananchi wametakiwa kufuatilia kwa karibu utabiri wa hali ya hewa wa kila siku, kila mwezi na tahadhari maalum zinazotolewa na TMA.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...