
Afisa Mtendaji Mkuu ALAF Limited, Bibhu Nanda (kulia), akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho wakati wa uzinduzi wa zoezi la siku mbili la utoaji wa elimu na upimaji wa afya kiwandani hapo.
Daktari wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani na Elimu kwa Umma kutoka Taasisi ya Kansa, Ocean Road, Dkt. Kandali Samwel, akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho wakati wa uzinduzi wa zoezi la siku mbili la utoaji wa elimu na upimaji wa afya kiwandani hapo.
KAMPUNI ya Alaf Limited, inayoongoza katika suluhisho mbalimbali za ujenzi, leo imezindua mpango wa siku mbili wa kuwaelimisha wafanyakazi kuhusu afya ikiwa ni moja wapo ya kipaumbele cha kampuni hiyo katika kujali afya na ustawi wa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo linalofanyika katika makao makuu ya ALAF jijini Dar es Salaam, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa kampuni hiyo, Bi.Hawa Bayumi alisema mpango huo ni sehemu ya dhamira ya ALAF ya ustawi wa wafanyakazi na uwajibikaji wa kijamii wa kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa Bi Bayumi, zoezi hilo ni la hiari na litazingatia upimaji wa Saratani ya Matiti, Saratani ya tezi dume na ile ya homa ya ini pamoja na chanjo ambapo alitoa rai kwa wafanyakazi kujitokeza ili kupima afya zao.
"Mpango huu unalenga kuelimisha wafanyikazi juu ya umuhimu wa kupima afya ambao ni pamoja kugundua mapema na hivyo kuzuia athari zinazoweza kujitokeza mapema ili kila mtu aweze kuishi maisha mazuri na yenye afya bora”, alisema.
Bayuni aliendelea kusema kuwa zoezi hilo ni bure kwa wafanyakazi wote na kwamba watumishi wote watapata muda wa kutosha wa kuwasiliana na kupata ushauri wa wataalam wa afya.
Pia alibainisha kuwa zoezi hilo litakuwa ni endelevu ili kuhakikisha wafanyakazi wanajenga utamaduni wa kupima afya zao ili waendelee kuwa na afya bora nje na ndani ya kazi.
"Wafanyakazi ni nguvu kazi muhimu kwa ajili ya kampuni yetu ndiyo maana uongozi umeona umuhimu wa kuandaa zoezi hili ili kila mfanyakazi aweze kujua hali yake ya kiafya ndani ya siku hizi mbili kwani afya nzuri ndiyo itawawezesha kuendelea na kazi vizuri”, alisema.
Aliendelea kusema kuwa kampuni ya ALAF itaendelea kuweka kipaumbele chake katika maswala ya afya na ustawi wa wafanyakazi wake kama sehemu ya juhudi zake zinazolenga kuifanya kampuni iwe na matokeo chanya kwenye mipango yake ya kazi.
ALAF Limited ni kampuni inayoongoza nchini Tanzania katika kuzalisha bidhaa kwa ajili ya shughuli za ujenzi zinazohusiana na maswala ya uezekaji wa paa kw akutumia bidhaa za chuma.
Madaktari kutoka Taasisi ya Kansa ya Ocean Road na Hospitali ya Hindu Mandal walifanya semina kadhaa na wafanyakazi kabla ya zoezi la upimaji na chanjo.
Kampuni hii Ilianzishwa mwaka wa 1960 na imeendelea kuwa taasisi muhimu katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo kupitia sekta ya ujenzi hapa nchini ambapo pia huzalisha bidhaa zingine ikiwemo koili na mabomba kwa ajili ya shughuli za ujenzi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...