Na Mwandishi Wetu, MBEYA
BENKI ya NMB, imeikabidhi ofisi ya Mkoa wa Mbeya hundi ya Sh. Milioni 30 kwa ajili ya udhamini wa maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa na sherehe za kitaifa za kuzima Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika Oktoba 14 mwaka huu jijini Mbeya.
Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Wogofya Mfalamagoha alimkabidhi hundi hiyo jana kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa wakati wa hafla iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Wogofya alisema udhamini huo ni mwendelezo wa benki hiyo wa kuunga mkono shughuli mbalimbali za serikali na kwamba fedha hizo ni kwa ajili ya kusaidia maandalizi ya sherehe hizo.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano ambayo mbio za Mwenge wa Uhuru zimefanyika, benki hiyo imetoa udhamini wa Zaidi ya Sh. Milioni 439.
Kupitia mfuko wetu wa kusaidia jamii, Benki ya NMB imejikita zaidi katika kutatua changamoto kwenye maeneo ya elimu, afya, na misaada ya hali na mali katika nyakati ngumu kama za majanga. Ni kwa zaidi ya miaka kumi mfululizo tumekuwa tukitenga asilimia 1% ya faida yetu kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayotunzunguka.
“Udhamini huu leo ni uthibitisho wa ushiriki wetu kwenye shughuli za maendeleo na kuhakikisha kwamba jamii inayotuzunguka inanufaika na faida ambayo tunaipata, juhudi zetu hizi za kusaidia jamii zimetufanya kutambulika na Jarida la Global Banking & Finance Magazine lenye makao yake New Jersey, Marekani kama Kinara wa Uwajibikaji kwa Jamii Tanzania 2025 vilevile jarida hilo limeweza kututambua kwa ubora wa huduma zetu kama Benki Salama Zaidi Nchini Tanzania,” alisema Mfalamagoha.
Alisema benki hiyo ina matawi 242 nchi nzima, mashine za kutolea fedha 720, Zaidi ya mawakala 60,000 na Zaidi ya wateja milioni 8.7 wanaopata huduma mbalimbali za kibenki.
Hata hivyo alisema ili kusogeza Zaidi huduma kwa wateja, benki hiyo imeanzisha masuluhisho mbalimbali ikiwemo huduma ya MshikoFasta ambayo ni huduma ya mikopo ya kidijitali, isiyokuwa na dhamana, kupitia simu ya mkononi ambapo mteja wanaweza kukopa kuanzia TZS 1,000 mpaka TZS 1,000,000.
Akipokea hundi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa aliishukuru benki ya NMB kwa udhamini huo alisema utasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya maandalizi ya sherehe hizo huku akizitaka taasisi zingine kuiga mfano huo.
Alisema benki ya NMB ni taasisi ambayo imekuwa ikishirikiana na serikali kwa kiasi kikubwa kwenye utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Malisa aliuomba uongozi wa benki hiyo kinara kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wawe na utamaduni wa kutunza fedha zao benki badala ya kuzitunza nyumbani au kwenye mifumo mingine isiyokuwa rasmi.
“Kwa niaba ya serikali ya mkoa nawashukuru sana benki ya NMB kwa udhamini huu, naomba taasisi zingine ziige mfano huu wa kurudisha sehemu ya faida kwa jamii,” alisema Malisa.
Alisisitiza wananchi wa Mkoa wa Mbeya kuendelea kuiamini benki ya NMB na kuhifadhi fedha kwenye benki hiyo huku akiipongeza kuwa ni miongoni mwa benki bora nchini.
Maadhimisho ya wiki ya vijana duniani yanafanyika kitaifa jijini Mbeya na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 14 mwaka huu siku ambayo pia itaambatana na maadhimisho ya miaka 26 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na uzimaji wa Mwenge wa Uhuru.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...