Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha Oktoba 20, 2025
ASHA Madamde, maarufu kama Bibi Hatibu mwenye miaka 120 ,mkazi wa mtaa wa Msufini, kata ya Sofu, Kibaha Mjini mkoani Pwani, amesisitiza kushiriki katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 huku akimuombea dua mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Dkt .Samia Suluhu Hassan.
Licha ya umri wake mkubwa wa miaka 120, Bibi Hatibu amesema kuwa afya yake na nguvu za Mungu zimemuwezesha kuendelea kushiriki katika shughuli muhimu za kijamii, ikiwemo kutimiza haki yake ya msingi ya kupiga kura.
Nyota ya mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kung'aa hadi kwa kundi la wazee, ambapo Bibi huyo alimwombea dua ya ushindi na kuwatakia mafanikio makubwa CCM katika kampeni ya nyumba kwa nyumba inayoongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Kibaha Mjini, Elina Mgonja, pamoja na kamati ya utekelezaji ya UWT.
“Nitapiga tiki, hilo halina mjadala,” alisema Bibi Hatibu akiwa anazungumza na Elina Mgonja nyumbani kwake, alipofikiwa na msafara wa UWT.
Bibi huyo alieleza kuwa amani ni tunu ya Tanzania, na uchaguzi ni suala nyeti kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Mimi ni shahidi wa historia ya nchi hii, nimeona mengi, wananchi wakapige kura kwa amani, kwa kuwa amani ni tunu ya nchi yetu, licha ya uzee wangu, naamini kila kura ina uzito mkubwa kwa hatma ya taifa hili, nimepiga kura tangu enzi za Uhuru na kwa majaliwa ya Mungu nitapiga tena mwaka huu,” alisisitiza bibi Hatibu.
Nae Elina Mgonja, Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini, alimshukuru Bibi Hatibu kwa dua yake kwa mgombea urais Dkt. Samia na kusema kwamba anastahili ushindi wa kishindo kutokana na kazi kubwa aliyofanikisha katika kipindi chake cha uongozi.
“Mama Samia ni nembo ya utendaji, miaka yake imeleta matumaini mapya, huduma bora na heshima kwa wanawake, wananchi hawana sababu ya kusita kumpa kura ya ndiyo!” alieleza Mgonja.
Kampeni za CCM zinaendelea kushika kasi katika Jimbo la Kibaha Mjini, ambapo CCM, jumuiya, mgombea ubunge Silvestry Koka pamoja na madiwani kupitia CCM, wanaendelea na mikutano na kampeni za nyumba kwa nyumba, lengo kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana na kueleza mipango ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025–2030.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...