TUME ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imekutana na wasimamizi na wafadhili wa programu ya utafiti ya u’Good!? kujadili utekelezaji wa programu mbalimbali za utafiti zinazolenga kuleta matokeo chanya kwa jamii, hususan katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mkutano huo umefanyika leo Oktoba 7, 2025, Dar es Salaam ukihusisha wafadhili kutoka Baraza la Utafiti la Afrika Kusini (NRF) na Shirika la BOTNAR la Uswisi, lengo likiwa ni kujenga jamii yenye ustawi hususani kwa vijana.
Programu hiyo inahusisha watafiti kutoka nchi 9 za ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara, Asia, Ulaya, na Amerika Kusini, ambao ni wanufaika wa mradi huo unaolenga kuchochea ustawi wa vijana na jamii kwa ujumla kupitia tafiti za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Utafiti wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Bugwesa Katale, amesema Tanzania ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huo kupitia ushiriki wake katika umoja wa mipango ya ruzuku za kisayansi unaoundwa na wanachama 17.
“COSTECH ilituma maandiko 120, ambapo 23 kati ya hayo yalishinda na kusaidia nchi kupata jumla ya miradi tisa itakayotekelezwa kwa ushirikiano na watafiti kutoka nchi tisa tofauti,” amesema Dkt. Katale.
Aidha, ameongeza kuwa programu hiyo ni muhimu kwa kuwa inaleta pamoja watafiti kutoka mataifa mbalimbali kufanya tafiti zitakazochochea hali bora ya maisha na ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maarifa na Mitandao ya Kitaasisi wa NRF Afrika Kusini, Dkt. Dorothy Ngila, amesema lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha bara la Afrika linapata nafasi ya kutoa sauti zake katika majukwaa ya kimataifa kuhusu jinsi ya kuzalisha maarifa mapya na kuunganisha vijana kupitia tafiti za pamoja.
“Tunataka bara la Afrika liwe na sauti moja kimataifa katika kutengeneza maarifa na mbinu bora za kusaidia vijana kustawi,” amesema Dkt. Ngila.
Naye Profesa Sharlene Swartz kutoka Human Sciences Research Council (HSRC) ya Afrika Kusini amesema wameamua kufadhili miradi 23 tofauti inayolenga kuchunguza uhusiano wa kijamii kati ya vijana na namna bora ya kujenga ustawi wa pamoja.
“Tunataka kuona vijana wanatumia tafiti hizi kuimarisha mshikamano na ustawi wa kijamii, si mafanikio ya mtu mmoja mmoja,” amesema Profesa Swartz.
Kwa upande wake, Dkt. Victoria Mwakalinga kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi amesema utafiti huo utakuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa sera mbalimbali, hususan zinazohusu maendeleo ya vijana wanaoishi vijijini, kwa kuangalia mbinu bora za uzalishaji wa mazao katika mazingira yanayokabiliwa na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo ambao umezinduliwa rasmi leo Oktoba 6, 2025, unatarajiwa kufungwa Oktoba 9, 2025, ukiwa na kaulimbiu isemayo: “Kustawi Pamoja, Ustawi wa Uhusiano wa Vijana kwa Mustakabali wa Kimataifa wa Kusini mwa Dunia.”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...