Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Arusha
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imefanya maboresho katika Kiwanja cha Ndege Arusha ambapo Sh.bilioni 17 zimetumika kufanya maboresho hayo ambapo kinatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
Akizungumza leo Oktoba 2,2025 mbele ya maelfu ya wananchi katika Uwanja wa Sheikh mkooani Arusha amesema katika miaka mitano iliyopita serikali imefanya maboresho makubwa katika viwanja vya ndege kikiwemo Kiwanja cha Ndege Arusha.
“Uwanja wa ndege Arusha kuanzia Januari mwakani utaanza kutumika usiku na mchana hivyo kusaidia safari za watalii, wafanyabiashara na hata wakazi wa mkoa huo na maeneo mengine nchini.
Dk.Samia amesema pia kiwanja kingine ndani ya mkoa huo ambacho kimefanyiwa maboresho ni kiwanja cha Ziwa Manyara kilichopo Karatu ambapo Sh.bilioni 8.5 kuweka mita 1500 za lami kujenga njia ya kuruka na kutua ndege.
Pia amesema marekebisho hayo yalihusisha ujenzi wa jingo la abira lenye uwezo wa kuhudumia abiria 150, eneo la maegesho lenye uwezo wa kuegesha magari 67 na kuweka lami katika barabara inayoingia uwanjani hapo.
Akizingumzia kuhusu kukuza utalii, amesema Serikali imeimarisha shirika la ndege Tanzania kwani katika kipindi cha miaka mitano ndege nane zimenunuliwa huku serikali ikiwa katika mpango wa kuongeza ndege zingine nane kuliwezesha shirika hilo kutanua wigo wake kuhudumia maeneo mbalimbali hivyo kukuza biashara.
Katika kukuza utalii ,Dk.Samia amesema pia wanafanyia vivutio vya utalii kuongeza watalii zaidi waje Tanzania huku akifafanua serikali inakwenda kujenga kituo cha mikutano ya kimataifa kipya baada ya kile cha AICC.“Kituo kipya cha mikutano kitakuwa na hotali, fursa zote za mikutano ndani ya jiji la Arusha. “
Pia amesema katika Wilaya Ngorongoro Oldonyo Lengai Serikali inakwenda kujenga vizuri kituo cha urithi wa jiolojia kwa watalii watakaopenda kutembelea maeneo ya kihistoria, kijiolojia, sayansi ambapo hicho ndicho kitakuwa kituo chao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...