Kongamano la Pili la Kitaaluma la BAASANA Afrika limezinduliwa rasmi jijini Arusha, likiwakutanisha wanazuoni na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kujadili namna elimu, sayansi, biashara na teknolojia zinavyoweza kuchangia kutatua changamoto za maendeleo barani Afrika.
Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mh. Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi, ameipongeza OUT kwa kuandaa jukwaa hilo muhimu la kubadilishana maarifa na tafiti.
“Tukio hili linaonesha hatua kubwa ya Tanzania katika kuunganisha wataalamu wa ndani na nje ya nchi ili kutafuta suluhisho za changamoto za kijamii na kiuchumi,” alisema.
Makamu Mkuu wa OUT, Profesa Alex B. Makulilo, amesema kongamano hilo ni fursa adhimu kwa wanazuoni kubadilishana tafiti na kuibua majibu ya changamoto zinazolikabili bara la Afrika.
“Kupitia kongamano hili, tunajifunza jinsi mbinu na tafiti za nchi nyingine zinavyoweza kutumika katika mazingira ya Tanzania na Afrika kwa ujumla,” alisema Prof. Makulilo.
Makamu Mwenyekiti wa BAASANA Global, Dkt. Chanaz Gargouri, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kitaaluma na kuchapisha tafiti zenye matokeo chanya kwa jamii.
Nae Mkuu wa kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii, Dkt. Dunlop Ochieng amebainisha kuwa kongamano hilo linahusisha wataalamu kutoka mataifa zaidi ya saba.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...