
Na.Mwandishi Wetu.
Serikali imesema itaendelea kuimarisha na kusimamia Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) ili viwe chachu ya kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, wakati wa uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa SACCOS kwa mwaka 2024 uliofanyika jijini Arusha.
Bw. Mwandumbya amesema wanachama wanapopata huduma za mikopo, hususan katika sekta binafsi, na kuzitumia kwenye biashara pamoja na shughuli za kiuchumi, huchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa pato la taifa.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, amesema kuwa ripoti inaonesha ukuaji wa Sekta ya Ushirika wa Akiba na Mikopo nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mali za SACCOS zimeongezeka kutoka Shilingi trilioni 1.32 mwaka 2023 hadi trilioni 1.46 mwaka 2024. Aidha, utoaji wa mikopo umeongezeka kutoka Shilingi trilioni 1.1 mwaka 2023 hadi kufikia trilioni 1.20 mwaka 2024.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wawakilishi wa taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya Kilimo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), SCCULT, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), COASCO, DSIK pamoja na viongozi wa SACCOS husika.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...