Ruvuma

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, amewataka wamiliki wa leseni za uchimbaji wa madini kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa jamii ili kuweka mazingira salama na yenye tija kwa shughuli za uchimbaji.

Dkt. Lekashingo alitoa wito huo Oktoba 2, 2025, wakati alipofungua mafunzo ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini na Wajibu wa Kampuni za Madini kwa Jamii (CSR) yaliyowashirikisha wadau wa sekta hiyo mkoani Ruvuma.

Alisema lengo kuu la mafunzo hayo lilikuwa ni kuhakikisha jamii inanufaika kiuchumi na kimazingira kutokana na shughuli za madini, sambamba na utekelezaji wa sera za maendeleo ya taifa.

“Msingi wetu ni kufanya kazi kwa haki, uwazi na kushirikiana na wadau wote ili rasilimali za madini ziwe nguzo ya maendeleo ya taifa na chanzo cha ustawi kwa kila Mtanzania,” alisema Dkt. Lekashingo.

Aidha, alisisitiza kuwa kupitia uwekezaji katika mafunzo, teknolojia za kisasa, ujenzi wa viwanda na uwajibikaji wa kampuni kwa jamii na mazingira, Tanzania itaweza kupata mageuzi makubwa katika Sekta ya Madini.

Alibainisha pia kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha Sekta ya Madini inachangia ipasavyo Pato la Taifa na kufungamanishwa na sekta nyingine za kiuchumi ili kuleta maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Dkt. Theresia Numbi, alisema mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 yameweka msisitizo wa kushirikisha Watanzania ipasavyo katika sekta hiyo.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ilisababisha kutungwa kwa kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania mwaka 2018 ambazo zimeendelea kufanyiwa maboresho.

“Matokeo ya maboresho hayo yamewezesha Watanzania wengi kupata ajira katika migodi, kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo, kuimarishwa kwa uhamishaji wa teknolojia na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu dhana ya ushirikishwaji,” alisema Dkt. Numbi.

Naye Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Jumanne Mwankhoo, aliishukuru Tume ya Madini kwa kupeleka mafunzo hayo mkoani humo kwa mara ya kwanza na kuahidi kuhakikisha mafunzo yaliyotolewa yanatekelezwa kikamilifu.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...