Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Katika kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2025, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa msaada wa vifaa vya kilimo, pembejeo na viuatilifu kwa kikundi cha vijana wa Wazito Farm Flex kinachojihusisha na kilimo cha mbogamboga na matunda (horticulture).
Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa TADB wa kurudisha kwa jamii (CSR) katika kuadhimisha wiki hiyo ambayo hufanyika kila mwaka wiki ya pili ya Oktoba.
Mbali na msaada huo, TADB pia imeandaa ziara ya mafunzo (Exposure Visit) kwa vijana wa Wazito Farm Flex visiwani Zanzibar, yenye lengo la kuwawezesha kujifunza na kubadilishana uzoefu na wenzao waliopiga hatua kubwa katika kilimo cha kisasa na biashara.
Kikundi cha Wazito Farm Flex kinaundwa na vijana saba waliohitimu vyuo vikuu mbalimbali nchini na kuunganishwa na dhamira ya kuwekeza katika kilimo biashara. Kikundi hiki kiliibuliwa na kulelewa na TADB kupitia programu ya TADB Mikoani, inayolenga kuwafikia wakulima hasa vijana na wanawake na kuwaelimisha juu ya fursa za sekta ya kilimo kupitia huduma za kifedha.
Tayari, kikundi hiki kimefanikiwa kuajiri vijana wengine 20 kutoka kijiji kinachozunguka shamba lao, hatua inayoongeza ajira na kuchangia kukuza uchumi wa jamii.














Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...