Mbinga, Ruvuma 

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ruvuma leo limefanya ziara maalum katika Wilaya ya Mbinga ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, kwa lengo la kutambua mchango wa wateja wake wanaotumia huduma ya umeme katika shughuli za uzalishaji na kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

Katika ziara hiyo TANESCO imekabidhi zawadi mbalimbali kwa wateja wake wakiwemo mama lishe waliopatiwa masufuria ya kisasa ya kupikia kwa umeme (pressure cookers), wajasiriamali wa saluni za kike na kiume waliopokea tokeni za LUKU, pamoja na shule ya sekondari ya Mbinga iliyozawadiwa umeme wa thamani ya shilingi laki moja kwa ajili ya kusaidia maandalizi ya mitihani ya taifa kwa wanafunzi wa bweni.

Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma Alan Njiro, amesema shirika hilo linatambua umuhimu wa kuwa karibu na wateja wake, hasa katika kipindi hiki ambacho serikali inapigia chapuo matumizi ya nishati safi, alibainisha kuwa utoaji wa masufuria yanayotumia umeme ni mkakati wa kusaidia wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo ni hatari kwa afya na mazingira.

“Masufuria haya yanatumia umeme kwa kiwango kidogo na ni rafiki wa mazingira, yamekusudiwa kuwasaidia mama lishe kupunguza gharama za uendeshaji na kuboresha huduma zao,”

Kadharika wanafunzi na walimu wa shule ya sekondari ya Mbinga wamepatiwa elimu juu ya matumizi salama na sahihi ya umeme, Njiro amesisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari kubwa pindi kunapotokea hitilafu, akiwataka wananchi kutoa taarifa kwa haraka kupitia namba ya bure ya huduma kwa wateja 180, badala ya kugusa nyaya zilizokatika au mtu aliyepigwa na umeme.

Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Mbinga, Mhandisi Edward Kweka, aliwahimiza walionufaika na vifaa hivyo hasa mama lishe, kuhakikisha wanavitumia kikamilifu kwa ajili ya shughuli zao za kila siku, amesema vifaa hivyo vinaokoa muda na gharama, sambamba na kuwa salama kwa afya zao.

Aidha ametoa wito kwa wateja wa TANESCO kuendelea kushirikiana na shirika hilo hasa panapotokea changamoto, akisisitiza kuwa TANESCO imeendelea kujitahidi kutoa huduma bora na za haraka kwa wateja wake.

Wakiwa na furaha baada ya kupokea masufuria ya kisasa ya kupikia kwa umeme, Regina Komba na Mama Sania ambao ni mama lishe katika stendi ya mabasi ya Mbinga, walitoa shukrani kwa TANESCO kwa kuwaona kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya kijamii, wamesema msaada huo utawapunguzia gharama kwani awali walitumia zaidi ya shilingi 1,000 kwa mkaa kupikia kilo moja ya mchele, lakini kwa sasa watatumia umeme wa chini ya shilingi 250 kwa kazi hiyo hiyo.

“Tumepewa elimu na sasa tunaelewa faida za kutumia umeme. Tutatumia masufuria haya kwa ufanisi na tukikutana tena mwaka mwingine, mtatukuta tunayatumia migahawani kwetu,”

TANESCO Ruvuma imeonesha dhamira ya dhati ya kushirikiana na jamii katika kuhamasisha matumizj ya nishati safi ya umeme ambayo ni salama, nafuu na rafiki kwa mazingira chini ya kaulimbiu ya wiki ya huduma kwa wateja isemayo "Mpango Umewezekana" wiki iliyoanza tarehe 6 mwezi oktoba 2025, na itahitimishwa tarehe 11 mwezi huu.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...