Na Miraji Msala, Kisarawe – Pwani

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani umeendelea kuboresha miundombinu ya barabara kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara na madaraja, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha uchumi wa wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo, kwa niaba ya Meneja wa TARURA Wilaya ya Kisarawe, Fundi Sanifu Mkuu Apolinary Rutaganya alisema miradi hiyo imekuwa kichocheo cha maendeleo na imechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha usafiri, biashara, na upatikanaji wa huduma muhimu katika maeneo ya vijijini.

Rutaganya alisema kuwa miongoni mwa miradi iliyotekelezwa ni ufunguaji wa barabara mpya ya Kisarawe–Kwembe yenye urefu wa kilomita 7.3, iliyotekelezwa kwa ufadhili wa mfuko wa jimbo kwa gharama ya shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Alisema kazi zilizofanyika ni pamoja na uwekaji wa makalavati, ujenzi wa daraja, na mifereji ya maji, ili kuhakikisha barabara hiyo inapitika kipindi chote cha mwaka.

Mradi huu ulitekelezwa na Mkandarasi Suma Company Ltd, ulianza tarehe 16 Juni 2023 na kukamilika tarehe 17 Desemba 2023, ikiwa ni ndani ya muda uliopangwa, na umekamilika kwa asilimia 100,” alisema Rutaganya.

Aliongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kumewezesha wananchi wa Kisarawe na maeneo jirani kupata huduma za afya kwa urahisi katika Hospitali ya Mloganzila, kutokana na kuwekwa kwa daraja jipya lililorahisisha usafiri na kupunguza gharama za usafirishaji.

Aidha, Rutaganya alibainisha kuwa mradi mwingine unaoendelea ni wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami inayounganisha Kimani na Chanika, wenye thamani ya shilingi milioni 468.33.

Mradi huu ulianza kutekelezwa tarehe 8 Agosti 2024 na unatarajiwa kukamilika tarehe 6 Desemba 2024. Hadi sasa umefikia asilimia 95 ya utekelezaji, ukiambatana na ufungaji wa taa 25 za barabarani kwa ajili ya kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara wakati wa usiku,” alifafanua.

Rutaganya aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia TARURA, akisema hatua hiyo imekuwa chachu ya mafanikio katika sekta ya miundombinu.

Tunaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutupatia fedha kwa wakati. Hii imetuwezesha kukamilisha miradi kwa viwango bora na ndani ya muda uliopangwa,” alisema.

Kwa upande wake, Apolinary George, mkazi wa Kisarawe, aliishukuru TARURA kwa juhudi hizo, akisema miradi hiyo imeondoa changamoto ya ubovu wa barabara iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

Hivi sasa tunafika hospitalini, sokoni na mashuleni kwa urahisi hata wakati wa mvua. Hii ni hatua kubwa ya maendeleo kwetu wananchi wa Kisarawe,” alisema George.

TARURA Kisarawe inaendelea kutekeleza miradi mingine ya kimkakati katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, ikiwemo matengenezo ya barabara za vijijini, ujenzi wa madaraja madogo na makalavati, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za usafiri kwa muda wote wa mwaka.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...