Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila akizungumza katika kongamano la PPPC lililofanyika Mkoani Iringa leo Oktoba 09, 2025.


Na Mwandishi Wetu. IRINGA
MKURUGENZI wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila amesema ubia baina ya sekta hizo mbili ni nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo na kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Nafasi ya PPP katika Kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Kafulila alisema mijadala na mapendekezo yaliyotolewa na washiriki yametoa mwelekeo thabiti wa namna Tanzania inaweza kutumia ubia wa sekta binafsi na umma kuharakisha maendeleo.

“Kongamano hili limeonesha wazi kuwa PPP sio ubinafsishaji, bali ni ushirikiano wa pande mbili unaolenga kuongeza ufanisi, kupunguza mzigo wa serikali, na kuhakikisha miradi ya kimkakati inatekelezwa kwa haraka zaidi kwa manufaa ya wananchi,” alisema Kafulila.

Katika majumuisho ya kongamano hilo, washiriki walisisitiza mambo kadhaa muhimu, ikiwemo:

1. Ubia wa umma na binafsi ni kichocheo kikuu cha maendeleo na utekelezaji wa Dira ya 2050.

2. PPP inalenga kupunguza mzigo wa kifedha kwa serikali, na kuiruhusu ijikite katika utoaji wa huduma muhimu za kijamii.

3. Ubia huo hauhusiani na ubinafsishaji, bali ni makubaliano ya muda yanayoweza kukoma kulingana na mazingira.

4. Sekta binafsi inaweza kufadhili miradi mikubwa ya kimkakati badala ya serikali kukopa fedha.

5. Hadi ngazi za halmashauri, PPP inaweza kutumika katika miradi kama masoko, maegesho na miundombinu midogo.

6. Elimu imetajwa kama eneo muhimu la ubia, ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaohitajika kufikia Dira 2050.

7. Mabadiliko ya mtaala wa elimu unaoegemea umahiri yanapaswa kuungwa mkono kwa uwekezaji katika kuwajengea walimu uwezo.

8. Elimu pia inapaswa kujikita katika maadili na thamani kwa wanafunzi.

9. Mawasiliano bora ya miradi ya PPP yanapaswa kuimarishwa ili jamii yote iwe sehemu ya utekelezaji.

10. Dira 2050 imekusudia kuimarisha ajira kwa vijana na kupunguza changamoto zao za kiuchumi.

11. Utekelezaji wa dira unahitaji utawala wa sheria, umoja wa kitaifa, ushirikishwaji, na mapambano dhidi ya rushwa.

12. Ili kujenga uchumi jumuishi, ni lazima kuongeza tija katika kilimo, ambacho ndicho tegemeo la Watanzania wengi, kwa kuboresha miundombinu ya umwagiliaji na uwekezaji vijijini.

Kafulila alihitimisha kwa kusema kuwa mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yatategemea kwa kiasi kikubwa ubunifu, ushirikiano wa wadau, na dhamira ya pamoja ya sekta zote mbili katika kuleta mageuzi ya kweli ya kiuchumi na kijamii.






Matukio mbalimbali katika kongamano PPPC lililofanyika Mkoani Iringa leo Oktoba 09, 2025.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...