Cape Town, 11 Novemba 2025: Airtel Africa, mmoja wa watoa huduma wakubwa wa mawasiliano na huduma za fedha kwa njia ya simu katika nchi 14 za Afrika, imemchagua Nokia kujenga mtandao wa kisasa wa mkongo wa mawasiliano (terrestrial fiber) wenye uwezo mkubwa unaounganisha nchi za Afrika Mashariki na Kati kupitia huduma yake ya hali ya juu ya fiber, Airtel Africa Telesonic.
Mradi huu wa kimkakati unalenga kuunganisha mataifa mbalimbali ya Afrika na kuzikutanisha na mkongo wa mawasiliano unaopita baharini na mifumo ya ardhini, hatua itakayoboresha kwa kiasi kubwa upatikanaji wa huduma bora za intaneti barani Afrika. Hatua hii inatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya jamii kwa kutoa huduma ya miundombinu ya kidijitali yenye ubora, uhakika na gharama nafuu.
Mradi huu, ambao ulitangazwa katika Mkutano wa 28 wa AfricaCom, wenye mkusanyiko mkubwa zaidi duniani wa viongozi wa sekta ya mawasiliano wanaolenga kutoa huduma katika nchi za Afrika, Mradi huu utawezesha mkongo wa mawasiliano wa ardhini na baharini wa 2Africa kuunganishwa moja kwa moja na mitandao ya ardhini, hivyo kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu na kwa kasi ya juu. Kupitia matumizi ya miundombinu ya fiber ya Telesonic pamoja na mifumo ya mkongo wa mawasiliano wa ardhini za baharini, mradi huu utatoa suluhisho la ongezeko la mahitaji ya data ya jumla (wholesale data) barani Afrika na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa kutumia teknolojia ya Nokia 1830 Photonic Service Switch (PSS), mtandao huu mpya utaweza kubeba hadi Terabiti 38 kwa sekunde (38 Tbps), hivyo kuwezesha usafirishaji wa data kwa kasi ya juu zaidi. Zaidi ya hapo, teknolojia hii imeundwa kuwa tayari kupokea maboresho ya C+L Band ili kuongeza uwezo wa mtandao. Mtandao wa DWDM unaojengwa, wenye jumla ya nodi 139 na kuunganisha nchi kadhaa, unaongozwa na mifumo ya kisasa ya Nokia ya Photonic Service Engine (PSE), ambayo ni ya kasi ya juu na yenye ubora wa kipekee.
Zaidi ya kujenga miundombinu ya kidijitali barani Afrika, mradi huu pia unaonesha dhamira ya Telesonic katika kuwawezesha wafanyabiashara, sekta ya elimu na huduma za afya kupata huduma bora za kidijitali.
Razvan Ungureanu, Afisa Mkuu wa Teknolojia wa Airtel Africa amesema: “Utekelezaji wa jukwaa la Nokia 1830 Photonic Service Switch, ni hatua muhimu sana katika kuboresha miundombinu yetu ya mtandao barani Afrika. Teknolojia hii itatuwezesha kuongeza uwezo wa mtandao na kutoa huduma za kasi ya juu zaidi ili kukidhi mahitaji makubwa ya matumizi ya intaneti. Kwa kutumia Photonic Service Engine ya Nokia katika mtandao wetu wa DWDM unaovuka nchi mbalimbali, tunafungua njia kwa maendeleo makubwa na fursa mpya barani Afrika.”
PD Sarma, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa Telesonic amesema: “Ushirikiano wetu na Nokia ni hatua muhimu katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali barani Afrika. Kupitia miundombinu hii ya kisasa kutoka Nokia, tunalenga kukidhi mahitaji ya data yanayoongezeka kila wakati barani. Mtandao huu utaendesha ukuaji wa uchumi, kuwawezesha wananchi, na kufungua fursa mpya kwa biashara na watu binafsi.”
Samer Lutfi, Mkuu wa Kundi la Ukuaji (Growth Group) la Miundombinu ya Mitandao ya Nokia kwa Mashariki ya Kati na Afrika amesema: “Tunajivunia kushirikiana na Airtel Africa Telesonic katika mradi huu mkubwa wa kuboresha upatikanaji wa huduma za intaneti barani Afrika. Teknolojia yetu ya DWDM yenye uwezo mkubwa na uthabiti wa hali ya juu imeundwa kusaidia taasisi na biashara kusukuma mbele mageuzi ya kidijitali na kukuza uchumi wa eneo hili. Mradi huu unadhihirisha dhamira yetu ya pamoja ya kuunganisha jamii na kuhimiza maendeleo.”



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...