
Na Mwandishi Wetu
MAWAKILI wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara, John Heche katika shauri la kushikiliwa kwa kiongozi huyo, wameiomba Mahakama iwape siku tatu kwa ajili ya kufanya utafiti na kujipanga kujibu pingamizi za upande wa Jamhuri.
Mawakili hao wakiongozwa na Selemani Matauka akisaidiana na mawakili Fredrick Msacky, Paul Kisabo, Neema Salum, Dorice Kafuku na Maduhu William, waliwasilisha mahakamani ombi kwa niaba ya Heche kuwataka wajibu maombi kumfikisha mahakamani au kumwachilia kwa dhamana.
Wajibu maombi ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (Inspector General of Police - IGP), Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu (Dar es Salaam - ZCO), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni (RCO), Kamishna Mkuu wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Kiongozi wa Mawakili hao, Matauka, aliomba siku hizo Novemba 10,2025 mbele ya Jaji Obadia Bwegoge baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Agatha Pima, kuieleza Mahakama kuwa wamewasilisha pingamizi la awali na pia wameshawapatia taarifa ya pingamizi waleta maombi.
"Upande wa wajibu maombi tulipewa nafasi ya kujibu kiapo kinzani, kwa sababu juzi ilikuwa Jumapili, waleta maombi tuliwapa taarifa ya kiapo leo (jana), lakini pia kabla hatujaendelea na kiapo kinzani, tumeleta pingamizi la awali," alidai Wakili Pima.
Baada ya maelezo hayo, Wakili Matauka alidai kuwa ni sahihi kwamba maombi yaliyokuwa mbele yake yaliitwa kwa ajili ya kusikilizwa na kwamba nusu saa iliyopita ndiyo alipewa taarifa hiyo ya kiapo kinzani na wajibu maombi.
"Ni maombi yetu kwa upande wa waleta maombi kwamba kwa sababu kuna pingamizi la awali, tungepewa nafasi ya kufanya utafiti na kujipanga. Naomba iahirishwe kwa ajili ya kwenda kujiandaa kujibu hoja za pingamizi, tunaomba siku tatu ambayo ni Novemba 13, 2025," aliomba Matauka.
Jaji Bwegoge aliuuliza upande wa wajibu maombi kuhusiana na ombi hilo, ambapo Wakili Pima alidai kuwa hawana pingamizi na kwamba wapewe muda wa kujiandaa.
"Waleta maombi wenyewe ndiyo wameomba muda, nahisi wanahitaji muda zaidi wa kujiandaa. Mahakama imeridhia ombi lao, na shauri litaendelea Novemba 13, 2025 saa 4:30 asubuhi," alisema Jaji Bwegoge.
Heche anashikiliwa na polisi tangu Oktoba 22, 2025, alipokamatwa nje ya geti la Mahakama Kuu Dar es Salaam.
Katika taarifa iliyotolewa na Wakili Hekima Mwasipu Novemba 4, 2025, ilieleza kuwa Heche amepewa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kigaidi kutoka Kimara hadi Magomeni na kujihusisha na vitendo vya kigaidi maeneo ya Msewe na External.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...