Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amewataka watumishi wa Tume kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara na kuepuka tabia zinazoweza kusababisha magonjwa sugu na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Mhandisi Lwamo ametoa wito huo Novemba 10, 2025, wakati akifungua mafunzo ya waelimisha rika wa Tume ya Madini yanayofanyika jijini Dodoma.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa miongoni mwa watumishi kuhusu VVU, Ukimwi na magonjwa yasiyoambukiza, ili kulinda afya zao na kuboresha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

“Afya bora ya mwili na akili ni nguzo muhimu ya utendaji kazi wenye tija. Magonjwa mengi tunayokabiliana nayo leo yanatokana na mitindo ya maisha, ulaji usio sahihi, kutofanya mazoezi na tabia hatarishi za ngono. Ni jukumu letu kila mmoja kuhakikisha tunajilinda na kuishi kwa afya,” amesema Mhandisi Lwamo.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa waajiri kujumuisha mikakati ya afya kazini kwenye mipango ya kila mwaka ya taasisi, sambamba na kujengeana uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiafya katika maeneo ya kazi.

Ameongeza kuwa Tume ya Madini imeendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa kuhimiza mazoezi ya viungo kupitia mabonanza, pamoja na kuhakikisha watumishi wenye magonjwa sugu wanapata lishe bora na huduma stahiki.

Akizungumza kuhusu usiri wa taarifa za kiafya, Mhandisi Lwamo amewataka watumishi kuheshimu faragha ya wagonjwa na kuhakikisha taarifa za afya zinatolewa kwa ridhaa ya mhusika pekee, ili kuepuka usambazaji wa taarifa zisizo sahihi.

“Ni muhimu wale walioathirika kutoa taarifa kwa hiari yao ili waweze kusaidiwa ipasavyo. Tunapaswa kuwa na moyo wa huruma na uelewa katika kushughulikia masuala haya,” ameongeza Mhandisi Lwamo.

Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye pia ni Fundi Sanifu wa Migodi kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi -Kahama, Jackson Mumanyi, ameishukuru Tume ya Madini kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu, akisema yatasaidia kuongeza uelewa na kubadili mitazamo ya watumishi kuhusu kujikinga na magonjwa hayo.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika katika ofisi za Tume ya Madini mkoani Dodoma, yakiwa na lengo la kuandaa waelimisha rika watakaosaidia kusambaza elimu ya afya kazini na kuhimiza tabia za kufanya mazoezi kwa watumishi wote wa Tume.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...