Katika kuadhimisha Siku ya Sayansi Duniani, Kijiji cha Makumbusho Jijini Dar es Salaam kupitia Nyumba ya Wazaramo kimeunganisha nguvu za sayansi na jamii kwa lengo la kuonesha namna elimu ya sayansi inavyoweza kusaidia kuhifadhi urithi wa kitamaduni na kujenga jamii endelevu yenye amani.
Tukio hilo limewakutanisha wanasayansi, wahifadhi wa makumbusho, wanafunzi na jamii ya Wazaramo ili kusherehekea mchango wa sayansi katika maendeleo ya kijamii na kiutamaduni.
Akizungumza katika maadhimisho hayo leo Novemba 10, 2025, Mhifadhi Mwandamizi wa Makumbusho ya Taifa (NMT), Bi. Sechelela Magoile, amesema kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuhusisha sayansi na jamii kwa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu maendeleo ya kisayansi, kukuza uelewa na kuweka jamii salama.
Bi. Magoile ameeleza kuwa katika maadhimisho hayo, NMT imewasilisha utekelezaji wa mradi wa “Ukuaji wa Miji na Kupotea kwa Urithi wa Kitamaduni wa Jiji la Dar es Salaam” ambao unalenga kuonesha historia ya asili ya kabila la Wazaramo – wazawa wa eneo la Dar es Salaam – na jinsi maisha yao ya kila siku yanavyohusiana na sayansi katika nyanja za afya, uhifadhi wa chakula na mazingira.
“Tumeita wanafunzi ambao ndio umri sahihi wa kuelewa walipotoka na wanakoelekea katika utamaduni wao,” amesema Bi. Magoile.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Makumbusho ya Taifa, Chuo Kikuu cha SMUS Technische, na wanajamii kutoka jamii ya Wazaramo.
Kwa upande wake, Afisa Uratibu wa Utafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Bw. Clavery Makoti, amesema ukuaji wa miji unaenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hali ambayo inaweza kuwa na athari chanya au hasi kwa utamaduni wa jamii.
“Ni vyema tukajikita kufanya tafiti katika eneo hili ili kupata taarifa sahihi za kisayansi zitakazoainisha ukubwa wa upotevu wa utamaduni na namna bora ya kulitatua,” amesema Makoti.
Ameongeza kuwa COSTECH ingependa kuona ukuaji wa miji unaoenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia yenye manufaa kwa utamaduni, si kwa jamii ya Dar es Salaam na Wazaramo pekee bali kwa makabila yote nchini.
“Tafiti za aina hii zitasaidia kuweka mizani kati ya maendeleo ya kisasa na uhifadhi wa urithi wa kitamaduni wa Tanzania,” amesisitiza.
Muandaaji wa Maonesho, Bw. Jackson Mwasha, amesema amekusanya taarifa kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo jamii, wataalamu wa NMT na wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kufanikisha maandalizi ya maonesho hayo kwa dhima iliyokusudiwa.
Naye Bw. Mgeni Ramadhani Bway, mjenzi wa nyumba za asili za kabila la Wazaramo, amewashukuru Makumbusho ya Taifa kwa kuwashirikisha wananchi katika tafiti hizo, akisema hatua hiyo itasaidia vijana kujifunza na kuilinda jamii yao.
“Kushirikishwa kwetu ni fursa kubwa kwa vijana kujifunza na kuona umuhimu wa kulinda tamaduni zetu,” amesema Bway.
Kwa upande wake, Vainess Jofrey, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbezi Ndumbwi, amesema kupitia maadhimisho hayo wamejifunza kuhusu utamaduni wa Kizaramo, ikiwemo maadili ya nidhamu, utii na ubunifu katika utengenezaji wa vifaa vya matumizi vinavyotokana na matawi ya mnazi.


















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...