Na-Mwandishi wetu Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amefanya ziara ya kikazi katika Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dodoma na kueleza kuridhishwa kwake na hali ya uhifadhi wa dawa, miundombinu pamoja na mazingira ya kazi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua bohari hiyo, Mhe. Senyamule amesema kuwa mazingira yaliyopo yanaendana na viwango vinavyotakiwa na yanatoa uhakika wa upatikanaji wa dawa kwa wakati katika hospitali na vituo vya afya.

“Nimefurahishwa sana na namna dawa zinavyohifadhiwa. Miundombinu ni mizuri na mazingira ni salama. Haya ni mazingira yanayotoa matumaini kwa wananchi kupata huduma bora za afya” amesema  Mhe. Senyamule.

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya afya hasa katika eneo la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba Nchini.

 “Haya ni mapinduzi makubwa katika eneo la uhifadhi wa dawa. Hili nililoliona leo ni ushahidi kwamba Serikali inaendelea kufanya mageuzi makubwa kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati kwenye hospitali na vituo vya afya,” aliongeza.

Kadhalika Mhe.  Senyamule amesema kuwa lengo la ziara yake limetimia baada ya kujionea akiba ya dawa, idadi ya vifaa tiba pamoja na miundombinu imara inayotumika kuhifadhi dawa.

 “Kuanzia mapokezi hadi mazingira ya kazi nimejiridhisha kuwa mmejipanga vizuri. 

Tuiamini Serikali kwa sababu mambo mazuri yanaendelea kufanyika,” alisisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri amesema kuwa uwepo wa dawa na vifaa tiba kwa wingi katika bohari hiyo ni ishara njema kwa wananchi wa Dodoma na mikoa jirani. 

“Nawapongeza kwa mazingira mazuri ya kazi, mmezingatia pia upandaji wa miti na bustani nzuri jambo linaloendana na mkakati wa kuikijanisha Dodoma. Dawa nilizoziona ndani zinatoa matumaini makubwa ya kupunguza uhaba wa dawa” alisema Alhaj Shekimweri.

Naye Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa alisema kuwa bohari hiyo imejikita katika misingi minne mikuu ya utendaji kazi ambayo ni utengenezaji, utunzaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba.

“Hadi sasa Kanda ya Dodoma tunahudumia jumla ya wadau 443, na kuanzia mwezi Juni tumefanikiwa kusambaza dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni 8.2” alisema Jumaa.

Ziara hiyo inaonesha juhudi za Serikali katika kufuatilia utekelezaji wa shughuli za kuimarisha mifumo ya afya Nchini, na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...