 Kuleta mapinduzi katika biashara na urahisi wa malipo kwa wateja na wafanyabiashara wa Tanzania.


 Vodacom Tanzania, kampuni inayoongoza katika huduma za mawasiliano nchini, imezindua rasmi huduma ya malipo ya kimataifa (M-Pesa Global Payments), hatua inayoleta mapinduzi katika biashara na urahisi wa malipo kwa wateja na wafanyabiashara wa Tanzania wanaosafiri na kufanya biashara nje ya mipaka ya nchi, Pia kuongeza ujumuishwaji wa kifedha kidigitali.

Kupitia ushirikiano na VISA, Alipay, Network International, Magnati na MTN Uganda, wateja sasa wanaweza kufanya malipo kwa kutumia mfumo wa Tap & Pay duniani kote kwa kugusisha simu yenye M-Pesa Visa card kwenye mashine ya malipo, kulipa wafanyabiashara nchini China kupitia Alipay kwa mfumo unaowezeshwa na Thunes, kufanya miamala Dubai kwa wafanyabiashara waliounganishwa kwenye mfumo wa TerraPay, pamoja na kuwalipa wafanyabiashara nchini Uganda moja kwa moja kwenye waleti zao za MTN MoMo., yote haya kupitia M-Pesa Super App au Menyu ya M-Pesa.

Huduma hizi ni salama, rahisi kutumia na zinaondoa changamoto zinazotokana na mifumo ya kibenki. Kwa pamoja, huduma hizi zimeifanya M-Pesa kuwa moja ya mifumo ya malipo ya kidigitali iliyoendelea zaidi barani Afrika. 

Uzinduzi huu unawawezesha wateja wa Tanzania na wasafiri wanaofanya malipo ya mara kwa mara katika uwanda wa Afrika Mashariki, Mashariki ya Kati, Asia na maeneo mengine duniani, lakini hukabiliana na gharama, ucheleweshwaji au ukosefu wa usalama kwa baadhi ya mifumo ya malipo.

Epimack Mbeteni, Mkurugenzi wa M-Pesa Vodacom Tanzania, alisema: “Ushirikiano wetu na VISA, Alipay, Network International na MTN Uganda unaonyesha dhamira yetu ya kujenga mifumo imara ya malipo ya kidigitali. Kwa pamoja, tunawawezesha watu kufanya malipo hata wavukapo mipaka ya Tanzania kwa urahisi ule ule wanaoufanya ndani ya nchi, kwa usalama, haraka na kwa gharama nafuu,” alisema Mbeteni. 

Mkurugenzi huyo aliongeza kwamba, “hili ndilo lengo kuu la M-Pesa: kuendeleza ujumuishwaji wa kifedha na kuhakikisha ubunifu wa kidigitali unaowanufaisha wajasiriamali wadogo, wa kati, wakubwa pamoja na wateja wenye mahitaji binfsi ya malipo. Kupitia nguvu hii ya pamoja, tunafungua njia mpya za biashara, kupunguza gharama za uendeshaji na kuwapa wateja uhuru mpana wa kushiriki katika uchumi wa kidigitali.”

Uzinduzi huu unaleta ubunifu mpya uitwao M-Pesa Tap & Pay kwa ushirikiano na Visa, ubunifu wa kwanza barani Afrika, unaowawezesha wateja kulipa duniani kote kwa kugusa tu simu zao zenye M-Pesa Visa card kwenye machine za watoa huduma zenye mfumo wa Visa. Victor Makere, Meneja wa Nchi wa Visa Tanzania, alisema: “Kupitia ushirikiano huu, tunawawezesha mamilioni ya wateja wa M-Pesa kufurahia malipo ya kidigitali yaliyo salama na rahisi popote Visa inapokubalika. 

Teknolojia ya Tap & Pay ni huduma inayomruhusu mteja kulipa kwa kugusisha simu yake karibu na mashine ya malipo yenye mfumo wa Visa, bila kuingiza namba ya kadi au PIN. Malipo yanakatwa moja kwa moja kupitia M-Pesa Visa card iliyopo ndani ya simu kidigitali. Hii inaongeza usalama na urahisi, ikiruhusu wateja kufanya malipo duniani kote bila kufichua taarifa zao nyeti. Ubunifu huu unaunga mkono safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa malipo ya kidigitali na kuwawezesha wateja na biashara kulipa kwa njia za kisasa zaidi.”

Kupitia Mtandao wa Thunes, wateja wa M-Pesa sasa wanaweza kulipa wafanyabiashara nchini China ndani wanaotumia mfumo wa Alipay kwa kasi na usalama.

 Andrew Stewart, Afisa Mkuu wa Mapato wa Thunes, alisema: “Urasimishaji wa malipo ya kuvuka mipaka kwa njia ya kidigitali ni hatua muhimu inayoongeza upatikanaji wa huduma na kusaidia dhamira yetu ya kuwawezesha mabilioni ya watumiaji kushiriki kikamilifu katika uchumi wa dunia. 

Kupitia ushirikiano wetu na Vodacom, sasa tunawezesha biashara za Tanzania kuwalipa wafanyabiashara wa China papo hapo kupitia mtandao wa Alipay. Kiwango hiki kipya cha uunganishaji na ubunifu kinaongeza imani katika mifumo ya kifedha ya simu na kufungua fursa mpya za biashara ya kimataifa”

TerraPay, ambayo inawezesha malipo ya kimataifa kwa wafanyabiashara, inawaruhusu watumiaji wa M-Pesa kufanya miamala na wafanyabiashara waliopo Dubai kupitia mtandao wao mpana wa malipo. 

Willie Kanyeki, Makamu wa Rais wa TerraPay Kusini mwa Jangwa la Sahara, alisema: “TerraPay tunaamini katika uunganishaji wa mifumo na kuwezesha malipo bila mipaka. Ushirikiano wetu na Vodacom unapanua fursa za biashara kwa njia salama, kwa Watanzania wanaofanya shughuli Dubai, na kuwaunganisha watumiaji wa Afrika na masoko mapya ya dunia.”

Kwa upande wa malipo kidigitali nchini Uganda kupitia MTN MoMo, MTN ina mchango muhimu katika kurahisisha biashara za kikanda kwa wajasiriamali wadogo na wa kati. Richard Yego, Mkurugenzi wa MTN Mobile Money Uganda, alisema: “Ushirikiano huu ni hatua muhimu kuelekea biashara huru na endelevu katika ukanda huu. 
Pamoja na Vodacom, tunafungua upatikanaji mkubwa wa huduma za kifedha kwa maelfu ya wafanyabiashara wanaovuka mipaka ya Uganda na Tanzania, hasa wale wa sekta ya biashara ndogo na za kati ambao ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu.”

Kwa kuzingatia matumizi makubwa ya huduma za fedha kwa simu na ongezeko la simujanja nchini Tanzania, masuluhisho haya ni nyenzo muhimu kwa wateja wa kawaida pamoja na biashara ndogo na za kati zinazohitaji huduma za kifedha za uhakika, za haraka na rahisi.

M-Pesa ikiendelea kupanuka kama huduma salama na rahisi ya malipo ya kimataifa, Vodacom Tanzania inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kujenga uchumi jumuishi wa kidigitali na kubadilisha maisha kupitia teknolojia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...