NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Dkt. Jim Yonazi, ameziagiza wizara zote nchini kuhakikisha zinadhibiti kikamilifu majanga ya moto katika majengo ya serikali kwa kutekeleza mikakati madhubuti ya kinga na tahadhari.
Ametoa agizo hilo wakati akifungua kikao maalum cha kujengea uwezo Wakurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka wizara mbalimbali, kilicholenga kuongeza uelewa kuhusu usimamizi wa majanga hususani moto mahala pa kazi.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Yonazi amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha hatua za kuzuia na kukabiliana na majanga ya moto zinachukuliwa mapema, ili kulinda maisha ya watumishi wa umma pamoja na mali za serikali.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, CGF John Masunga, amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 jeshi hilo limepokea jumla ya matukio 2,517 ya moto, ambapo matukio 33 yalihusu majengo ya serikali ikiwemo shule, ofisi na masoko sawa na asilimia 1.31 ya matukio yote. Amesema takwimu hizo zimechochea umuhimu wa kutoa mafunzo hayo kwa watumishi wa serikali ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na majanga.
Kamishna Masunga ameongeza kuwa pamoja na uwepo wa vifaa na mifumo ya kisasa ya kuzima moto katika majengo ya serikali, bado mafunzo ya mara kwa mara kuhusu matumizi sahihi ya vifaa hivyo ni muhimu. Amefafanua kuwa mafunzo hayo yatawasaidia watumishi kutambua njia salama na mbinu za kujinusuru endapo moto au tukio lingine la dharura litajitokeza.
Aidha, amebainisha kuwa kati ya mwezi Julai hadi Septemba 2025, zaidi ya majengo 438 ya serikali yalifanyiwa ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto hata hivyo ukaguzi huo ulibaini changamoto kadhaa ikiwemo majengo kutokidhi viwango vya usalama kama vinavyoelekezwa na sheria na kanuni za usalama wa moto.
Changamoto nyingine zilizotajwa ni pamoja na miradi ya serikali kukamilishwa bila ushirikishwaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika hatua za majaribio ya mifumo ya kuzima moto, baadhi ya wizara kutojumuisha bajeti za ukarabati wa mifumo ya moto, pamoja na ujenzi wa majengo bila kuwasilisha michoro kwa jeshi hilo ili kupata ushauri wa kitaalam kabla ya ujenzi kuanza.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...