Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imetakiwa kutumia mbinu za kisasa za uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu za utafiti, kuchunguza na kutoa elimu ya uadilifu kwa umma ili kupunguza mmomonyoko wa maadili nchini.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) wakati wa ziara yake ya kikazi  katika ofisi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Makao Makuu jijini Dodoma tarehe 26 Novemba, 2025 ikiwa ni  mara yake ya kwanza kutembelea Taasisi hiyo tangu alipoteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongoza wizara hiyo. Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri aliambatana na Naibu Waziri Mhe. Regina Qwaray (Mb).

“Shirikianeni na Taasisi nyingine za Utawala Bora nchini kufanya utafiti wa hali ya maadili nchini na kutoa elimu ya uzalendo kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kupunguza mmomonyoko wa maadili, “ amesema.

Aidha Mhe. Kikwete ameiagiza Sekretarieti ya Maadili  kutowaonea  aibu Viongozi wa Umma wanaolalamikiwa kukiuka maadili kwa sababu ni jukumu lake kufuatilia tabia na mienendo ya Viongozi nchini.

“Sekretarieti ya Maadili ni msumeno wenye ncha kali, utumieni kuongeza uadilifu nchini kwa kutafuta ushahidi wa ukiukaji wa maadili miongoni mwa Viongozi wa Umma, waiteni  wanaokiuka maadili na wakemeeni wanaobainika kukiuka misingi ya maadili kwasababu hili liko katika mamlaka yenu,” amesema Mhe. Kikwete.

“Mmesema hapa kuwa kuna baadhi ya viongozi wana hofu ya kujaza Tamko kwa njia ya Mtandao, hili sio tatizo la Serikali, mmesha weka mifumo ya kupokea Tamko la Rasilimali na Madeni hakikisheni Viongozi wote wanajaza ifikapo tarehe 31 Desemba kwa mujibu wa sheria,”  amesisitiza.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma ni chombo  imara na kinaaminika hivyo kinatakiwa  kufanya kazi kwa kutenda haki kinapotekeleza majukumu yake ya kimsingi katika kusimamia na kukuza maadili kwa Viongozi wa Umma nchini.

“Hivi karibuni, Serikali na viongozi wamechafuka, Sekretarieti ya Maadili mnalo jambo la kufanya, msiwaogope viongozi kuwawajibisha pale wanapokiuka maadili,” alisisitiza Mhe Kikwete.

Awali akimkaribisha Waziri Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi ameeleza kuwa Sekretarieti ya Maadili katika kutekeleza majukumu yake, inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kukosekana kwa ushahidi wa baadhi ya malalamiko ya ukiukwaji wa maadili kwa baadhi ya Viongozi kutokana na baadhi ya mashahidi kutotaka kutoa ushahidi mbele ya Baraza la Maadili.

Katika hatua nyingine, Mhe Mwangesi ameeleza kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inatarajia kuanzisha ofisi za  Mikoa ili kusogeza huduma kwa Viongozi wa Umma na wananchi hasa utoaji wa elimu ya Mgongano wa Maslahi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...