Na Mwandishi Wetu

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Amos Pallangyo, leo amezindua Shindano la Mawazo Bunifu ya Biashara kwa mwaka wa masomo 2025/2026, shindano litakalofanyika katika Kampasi zote za TIA nchini.

Shindano hili linatarajia kutambulisha washindi watatu kutoka kila kampasi, huku washindi wa kwanza wakipata fursa ya kipekee ya kushiriki ziara ya kimafunzo nchini Afrika Kusini katika Chuo Kikuu cha Pretoria na Chuo Kikuu cha UNISA. Ziara hii itawapa wanafunzi fursa ya kujifunza, kupata uzoefu, na kuimarisha ubunifu wao kupitia ushirikiano wa kimataifa.

“Mashindano haya yatawakutanisha vijana wenye ndoto, ubunifu na ujasiri wa kufikiria nje ya mipaka. TIA tunahimiza ubunifu kwa kuwa ndio msingi wa biashara, na wabunifu ndio watakaosaidia taifa letu kusonga mbele katika uchumi wa kisasa.”. Alisema Profesa Pallangyo

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitalaam, Profesa Momole Kasambala, amesema shindano hili limeanza mwaka wa masomo 2023/2024 na limepata mafanikio makubwa. Katika miaka miwili iliyopita, TIA imejivunia kuona mradi wa bunifu mbalimbali ukiingizwa sokoni na wengine kushiriki maonyesho ya kitaifa na kimataifa, ikiwa ni pamoja na maonesho ya Sabasaba.

Miongoni mwa bunifu zilizofanikiwa ni DALA App, ambayo imezaa kampuni tanzu ya Dala Real Estate, pamoja na Utagy, SMG Office, Sokoni Pro, utengenezaji wa batiki za kisasa zinazouzwa hadi nje ya nchi, na utengenezaji wa sabuni za kufulia na kuogea. Bidhaa hizi zimewawezesha wanafunzi kuanzisha biashara zao binafsi na kujiajiri.

Aidha, Dkt. Elimereck Akyoo, Mkurugenzi wa Kampasi ya Kigoma, ameeleza mafanikio ya Ukuzaji na Uendelezaji wa Wanafunzi Kitaaluma na Kitaalam, akisema wanafunzi wamepata mafunzo muhimu kuhusu usajili wa biashara kupitia BRELA, matumizi ya Ajira Portal, ujasiriamali, na urasimishaji wa bunifu kupitia SIDO, pamoja na namna ya kupata Passport kwa njia ya mtandao kupitia Idara ya Uhamiaji,

“Zaidi ya wanafunzi 650 walishiriki mafunzo ya ujasiriamali kupitia JA DEEP, huku 517 wakiweka mafanikio ya kumaliza mafunzo na kupatiwa vyeti,”. Alisema Dkt.Akyoo

Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi TIA Kigoma, Getruda Sendama, amesema uwepo wa kitengo cha Ukuzaji na Uendelezaji wa Wanafunzi Kitaaluma na Kitaalam umekuwa chachu ya fikra chanya, kuondoa dhana ya kutaka kuajiriwa tu, na kuhimiza kujiajiri kupitia mawazo ya biashara ya kiubunifu.

Uzinduzi huu unaonesha dhamira ya TIA ya kuendeleza ubunifu na kuandaa viongozi wa baadaye, huku ikiwapa wanafunzi fursa za kitaaluma na kibiashara zinazowawezesha kufikia malengo yao na kuchangia maendeleo ya taifa.
Afisa Mtendaji wa (TIA)Profesa William Amos Pallangyo akiongea na Wanafunzi wakati wa Uzinduzi wa Mashindano ya Wazo Biashara uliofanyika jijini Dar es Salaam
Profesa Momole Kasambala Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Tafiti na Ushauri wa Kitaalam akiongea na Wanafunzi wakati wa uzinduzi huo.
Dkt. Elimereck Akyoo Mkurugenzi Kampasi ya TIA Kigoma akizungumza katika uzinduzi huo
Makamu wa Rais Serikali ya Wanafunzi Kampasi ya Kigoma Getruda  Sendama akizungumza katika uzinduzi wa Wazo Biashara

Baadhi ya wanafunzi wa TIA walioshiriki Wazo Biashara

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...