Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeendelea kufanya mageuzi makubwa katika kuboresha upatikanaji wa  huduma ya umeme nchini hatua ambayo imeongeza imani na fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo Novemba 22, 2025, mkoani Dodoma katika kikao chake na viongozi wa TANESCO chenye lengo la kufanya tathmini na kukumbushana majukumu muhimu ya kuwahudumia wananchi. Ameutumia mkutano huo kuwataka watendaji wa TANESCO kuongeza kasi na ubunifu katika kuwaunganishia wananchi umeme kama sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Misheni 300.

Amesema kuwa ili mpango huo utekelezeke ipasavyo, ni lazima kuwachukulia  hatuaza kisheria  wakandarasi wote watakaobainika kuwa wazembe au kushindwa kuendana na kasi ya serikali ya kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na huduma ya umeme.

“Nawapongeza TANESCO kwa kazi kubwa na nzuri ya kuwafikishia wananchi huduma ya umeme, lakini bado tuna kazi kubwa mbele yetu. Ongezeni ubunifu na mbinu bora za kuwaunganishia wananchi umeme kwa haraka. Ninaamini tukishirikiana na wadau wetu, tutafikia lengo la kuwaunganishia wateja milioni 1.7 kwa mwaka,” alisema Mhe. Ndejembi.

Naye Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Makamba amemshukuru Rais.  Dkt.  Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika miradi ya umeme ambayo imekuwa na dhamira ya dhati ya  kuhakikisha wananchi wote mijini na vijijini wanafikiwa na huduma ya umeme.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhe. Felchesmi Mramba, amesema TANESCO imekuwa ikitekeleza miradi yake kwa viwango vya kimataifa, hatua inayofanya Tanzania kuwa kielelezo kwa mataifa mengine katika ujenzi na usimamizi wa miradi ya umeme.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Mhe. Balozi Zuhura Bundala, amesema  Shirika hilo lina watendaji wazalendo na wenye kujituma, ambao wanaendelea kufanya kazi kwa bidii  ambapo amesisitiza bodi hiyo itaendelea kushirikiana na Shirika ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema  katika kipindi cha siku 100 za utendaji wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Shirika litakamilisha miradi ya umeme  kwa kasi zaidi, ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa jua wa Kishapu ambao kwa sasa umefikia asilimia 83 ya utekelezaji.

“Katika kipindi cha siku 100 za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumejipanga kuhakikisha baadhi ya miradi ya umeme inakamilika, ukiwemo mradi wa umeme wa jua wa Kishapu. Pia tunaendelea na mkakati wa kuwaunganishia wananchi umeme  lengo ni kuwafikia wateja milioni 1.7 kwa mwaka,” alieleza Bw. Twange.

Kikao kazi hicho  kimehusisha viongozi wa ngazi ya juu wa TANESCO, wakurugenzi wa kanda, mameneja wa mikoa na wilaya, na kilifunguliwa rasmi na Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius  Ndejembi ambaye aliambatana na Naibu waziri wa nishati Mhe. Salome Makamba





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...