Msimamizi wa Msongo wa Kilovoti 220 kwa mikoa ya Njombe na Ruvuma Mhandis Liberatus Juma, , amewataka wananchi kutofanya shughuli za kibinadamu karibu na maeneo ya miundombinu ya umeme wa gridi ya Taifa, akisema kuwa ni kitendo hatarishi kinachoweza kusababisha vifo, uharibifu wa mali na kusababisha kukatika kwa huduma ya umeme katika maeneo mengi.

Akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa wananchi wa Kijiji cha Mbangamawe, Injinia Juma alisema kuwa maeneo ya umeme mkubwa wa msongo wa kilovoti 220 ni eneo tengefu lililotengwa maalumu kwa ajili ya shughuli za umeme pekee, hivyo wananchi hawapaswi kulima, kufuga au kufanya shughuli zozote kwenye eneo hilo.

Injinia Juma alifafanua kuwa kufanya shughuli katika eneo hilo kunaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo vya watu, mifugo, au kuungua kwa mali, kutokana na hatari ya kuangukiwa na nguzo za umeme.

Katika maelezo yake, alisema kuwa uharibifu wowote unaotokea kwenye nguzo za umeme unaweza kuathiri upatikanaji wa umeme kwa mkoa mzima, akitoa mfano wa vijiji vya Mshangano, Tanga na Mageuzi, ambako baadhi ya wananchi walihujumu miundombinu kwa kung'oa senyenge, kitendo kilichopelekea nguzo kupoteza uthabiti na kuanza kuanguka, na hivyo kuhatarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo kadhaa.

Amesema Kutokana na matukio hayo, TANESCO imeanza kutoa elimu mapema ili kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa kulinda miundombinu ya gridi ya Taifa, ambapo wameingia mkataba wa ulinzi shirikishi na vijiji vinavyozunguka miundombinu hiyo ili kuongeza ulinzi, ambapo katika eneo la Mbangamawe kuna zaidi ya nguzo 30, zinalipiwa huduma ya ulinzi kwa kiasi cha zaidi ya shilingi laki 7, fedha ambazo zinakwenda moja kwa moja kwenye kijiji na kuwasaidia wananchi kunufaika kiuchumi kupitia uwepo wa miundombinu hiyo.

Injinia Juma alisema kuwa kutokana na idadi ndogo ya watumishi wa TANESCO, haiwezekani kulinda miundombinu yote peke yao, hivyo wajibu wa kulinda mali za umma ni wa kila mwananchi.

Katika kuhakikisha wananchi wananufaika na uwepo wa miundombinu ya umeme, kazi za usafishaji wa maeneo ya gridi zimekuwa zikipewa kipaumbele kwa wananchi wa vijiji husika ili kujipatia kipato na kujenga uhusiano mzuri kati ya shirika na jamii.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma Alan Njiro, aliwataka wananchi kutoa taarifa mara moja pindi wanapowaona watu wanaohujumu miundombinu au mtu yeyote anayepanda kwenye nguzo bila kuwa na kitambulisho cha TANESCO , amewataka kutoa taarifa zinaweza kwa uongozi wa kijiji au kupiga namba 180 bila malipo ili kuripoti moja kwa moja kwa shirika.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mbangamawe waliiomba TANESCO kuhakikisha watumishi wake wanatambulika kwa urahisi ili kusaidia kuwatofautisha na wahalifu wanaotumia mwanya huo kuiba au kuharibu miundombinu. Pia waliomba shirika kuhakikisha umeme unapatikana muda wote ili kuendelea kufurahia huduma muhimu zinazotegemea nishati hiyo.

TANESCO imeahidi kuendelea kutoa elimu na kuimarisha ulinzi ili kuhakikisha umeme unapatikana bila kukatika na miundombinu inabaki salama kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.




Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...