Na Mwandishi Wetu, Pugu–Kazimzumbwi
Tanzania imeendelea kujijengea heshima kimataifa katika usimamizi endelevu wa misitu baada ya kupokea ujumbe wa wataalamu wa misitu kutoka Jimbo la Yunnan, nchini China, waliowasili nchini kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kubadilishana uzoefu na utaalamu wa uhifadhi.
Ujumbe huo, ulioanza ziara yake Novemba 11 na unatarajiwa kumalizika Novemba 14, 2025, leo Jumatano umetembelea Msitu wa Hifadhi wa Pugu–Kazimzumbwi, uliopo wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani, kujionea mbinu mbalimbali za uhifadhi na ushirikishwaji wa jamii katika kulinda rasilimali za misitu.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Gerald Otieno, alisema ujio wa wageni hao ni sehemu ya juhudi za TFS za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya uhifadhi na maendeleo ya misitu na nyuki.
“Misitu ni sayansi. Sayansi hii inahitaji kubadilishana taarifa, wataalamu na maandiko. Wageni wetu wamekuja kujifunza kutoka kwetu jinsi tunavyosimamia misitu, nasi pia tunajifunza mbinu bora kutoka kwao,” alisema Otieno.
Aliongeza kuwa TFS imekuwa kituo cha kujifunzia kwa mataifa mengi kutokana na mbinu shirikishi inazotumia, ikiwemo kuhusisha jamii katika uhifadhi, jambo lililowavutia zaidi wageni hao.
“Walifurahishwa kuona jamii ikishiriki moja kwa moja katika ulinzi wa misitu, hasa maeneo yenye thamani ya kiutamaduni na kiutalii. Wameona jinsi tunavyohusisha mila, tambiko na utalii wa kiikolojia kama sehemu ya uhifadhi endelevu,” aliongeza.
Kwa upande wake, Jianga Rui, mwakilishi wa ujumbe wa Hunan Forestry Delegation kutoka Yunnan, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika uratibu wa taasisi za uhifadhi na usimamizi wa misitu.
“Tanzania ina hifadhi na misitu mikubwa zaidi kuliko sisi, lakini mna mfumo thabiti wa usimamizi wa wima unaorahisisha uratibu na uwajibikaji. Tunataka kujifunza kutoka kwenu na kuona namna tunaweza kuboresha mifumo yetu nyumbani,” alisema.
Jianga Rui alibainisha kuwa katika jimbo lao, mifumo ya usimamizi wa misitu kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na migongano ya kimaslahi, na kupitia ushirikiano huu wanatarajia kujifunza mbinu bora za kuunganisha maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.
Wakati wa ziara hiyo, ujumbe huo ulipata maelezo kuhusu historia ya Msitu wa Pugu–Kazimzumbwi, ikiwemo maeneo ya tambiko, vivutio vya kiasili, mimea na wanyama wa kipekee wanaopatikana humo.
Baada ya ziara hiyo, ujumbe huo unatarajiwa kuelekea Dodoma kwa ajili ya kikao cha majumuisho na mazungumzo na Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu, Prof. Dos Santos Silayo, yatakayolenga kuweka mpango mkakati wa muda mrefu wa ushirikiano katika tafiti na mafunzo ya uhifadhi.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...