Na Pamela Mollel, Arusha.
Mkutano wa kimataifa wa teknolojia ya akili bandia (AI) unaofanyika jijini Arusha umeendelea kuvuta wadau mbalimbali wa sekta ya TEHAMA, serikali na taasisi za huduma za umma, wote wakiwa na lengo la kujadili namna AI inaweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha utendaji wa taasisi za Afrika.
Akizungumza kwenye mkutano huo, mtaalam wa TEHAMA Eliya Kinshaga, amesema AI imekuwa kichocheo muhimu katika mageuzi ya kiteknolojia duniani, hivyo mataifa ya Afrika yanapaswa kuweka mazingira wezeshi, sera thabiti na mafunzo kwa wataalamu ili kunufaika ipasavyo na teknolojia hiyo. Amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya AI yanaweza kupunguza gharama za huduma, kuongeza ufanisi na kuimarisha usalama wa mifumo ya serikali na taasisi binafsi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Takwimu wa Benki Kuu ya Uganda, Bi Nalukwago Milly amesema taifa hilo limeanza kunufaika na AI kwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rekodi, ufuatiliaji wa miamala na kufanya maamuzi ya kiuchumi kwa tahadhari na usahihi zaidi. Amebainisha kuwa matokeo hayo ni ushahidi kuwa AI inaweza kuboresha taasisi za kifedha endapo itawekewa misingi madhubuti ya matumizi.
Aidha, mwakilishi kutoka Wizara ya Kilimo Kenya Haron kertish amesema AI imechangia kurahisisha usajili wa wakulima, utoaji wa mbolea na uchambuzi wa takwimu za uzalishaji, akisisitiza kuwa sekta ya kilimo inapata ufanisi mkubwa pale teknolojia inapowekwa mbele na kutumiwa kisayansi.
Wadau wa mkutano huo wamehitimisha kwa kusisitiza kuwa Afrika ina uwezo mkubwa wa kuongoza mageuzi ya AI endapo serikali na sekta binafsi zitawekeza katika ubunifu, utafiti na ushirikiano wa kikanda kwa maslahi ya uchumi wa bara zima.
Akihitimisha mjadala huo, Faustin Mgimba, mwanzilishi wa Scan Code, amesema Afrika haina budi kuongeza uwekezaji katika teknolojia zinazotengenezwa barani ili kupunguza utegemezi wa mifumo ya nje. Amesema mifumo ya ndani imeanza kuonyesha matokeo chanya kwenye taasisi mbalimbali, na kwamba ubunifu, sera bora na ushirikiano wa sekta zote ni msingi muhimu kwa bara kujenga mfumo madhubuti wa AI unaoendana na mahitaji ya kiuchumi ya Afrika.



.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...