

Access Bank Tanzania imezindua rasmi Access Wezesha, jukwaa jipya linalolenga kuwawezesha vijana wa kizazi kijacho kupata maarifa muhimu ya uelewa wa masuala ya fedha. Benki imeshirikiana na AIESEC IFM kuendesha mafunzo ya kina ya elimu ya fedha kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, ambapo zaidi ya vijana 200 walihudhuria ili kujifunza kuhusu akiba, upangaji bajeti, na kukuza tabia bora za usimamizi wa fedha.
Hatua inaonyesha dhamira ya Access Bank katika kuongeza ujumuishwaji wa kifedha na kuwawezesha vijana kupitia elimu na huduma rafiki za kibenki. Kupitia ajenda hii, Benki pia imeunda Akaunti ya IZE, akaunti mahsusi kwa vijana itakayo wasaidia wanafunzi kusimamia fedha zao kwa urahisi na uwajibikaji.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Irene Mutiganzi, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano ya wa Kampuni katika Access Bank Tanzania, alisisitiza umuhimu wa kuwafundisha vijana masuala ya fedha mapema.
“Kuwawezesha vijana kupitia elimu ya fedha ni hatua muhimu katika kuhakikisha mustakabali wao. Wanapofahamu namna ya kuweka akiba, kupanga bajeti, na kusimamia fedha zao kwa uwajibikaji, wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufikia malengo yao. Ushirikiano wetu na AIESEC IFM unaonyesha dhamira yetu ya kuunga mkono ukuaji na maendeleo ya vijana nchini,” alisema.
AIESEC IFM, Ni tawi la shirika linalojikita katika kukuza uwezo wa uongozi kwa vijana kupitia uzoefu wa vitendo, liliweka wazi kuwa mpango huu unachangia kwa kiwango kikubwa katika kuandaa viongozi wa baadaye wenye uwezo na maarifa sahihi.
Akizungumza katika tukio hilo, Faith Jonas Kwayu, Rais wa Tawi la AIESEC IFM, alisema:
“Ushirikiano huu na Access Bank unaendana kikamilifu na dhamira yetu ya kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto za dunia halisi. Uelewa wa fedha ni msingi muhimu wa uongozi wenye uwajibikaji na ukuaji binafsi. Tunajivunia kuona vijana wengi wakichukua hatua hii kuelekea kujenga maisha salama na yenye uwezeshaji.”
Mafunzo hayo yalijumuisha vipindi shirikishi, mazoezi ya kupanga bajeti, na majadiliano yaliyolenga kuwasaidia washiriki kufanya maamuzi sahihi ya kifedha. Access Bank na AIESEC wamethibitisha tena dhamira yao ya kuendeleza programu kama hizi katika maeneo mbalimbali nchini katika juhudi za kuunga mkono maendeleo ya vijana.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...