BANJUL, Gambia — Desemba 2, 2025
Afrika imepata uongozi mpya wa kusimamia rasilimali za misitu na wanyamapori baada ya Ebrima Jawara, Katibu Mkuu Wizara ya Mazingira ya Gambia, kuchaguliwa kwa kauli moja kuwa Mwenyekiti wa Mkutano wa 25 wa Tume ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWC25) na Wiki ya 9 ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWW9) kinachoendelea Banjui, Gambia.
Anachukua nafasi ya Prof. Dos Santos Silayo, Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ambaye alipongezwa na wajumbe kwa uongozi wake katika kipindi kilichotawaliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ukataji misitu na migogoro ya matumizi ya ardhi.
Uchaguzi huo, ulioongozwa na Edward Kilawe, Katibu wa Tume kutoka Ofisi ya FAO Kanda ya Afrika, ulihusisha wajumbe kutoka zaidi ya nchi 45 na kupewa uzito mkubwa kutokana na umuhimu wake katika kulinda misitu, kuimarisha takwimu za ufuatiliaji na kuongeza ushiriki wa jamii.
Akifungua mchakato wa uchaguzi, Kilawe alieleza alieleza utaratibu wa kugawa nafasi za uongozi kwa kanda nne za Afrika. Rwanda iliidhinishwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa Kanda ya Afrika Mashariki, hatua iliyoungwa mkono na Sudan Kusini.
Katika Kanda ya Kusini, Afrika Kusini ilimteua Bi. Pumeza Nodada, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mazingira, Misitu na Uvuvi, huku pendekezo la Zimbabwe likisababisha mashauriano ya faragha kabla ya kufikiwa kwa mwafaka.
Kanda ya Afrika ya Kati iliunga mkono kwa wingi uteuzi wa Chad, hatua iliyotafsiriwa kama ishara ya umoja na mshikamano wa kikanda.
Aidha, wajumbe waliidhinisha uteuzi wa Bi. Munchan kutoka Burkina Faso kuwa mwandishi wa taarifa, hatua inayoendeleza msukumo wa kuongeza usawa wa kijinsia katika nafasi za kiufundi.
Katika hotuba yake ya kuhitimisha uenyekiti, Prof. Silayo aliwataka viongozi wa bara hilo kuimarisha matumizi ya mifumo ya kisayansi, ubunifu na ushirikiano wa kikanda ili kukabili kasi ya ukataji misitu, kupungua kwa bioanuwai na kuongezeka kwa migongano kati ya binadamu na wanyamapori.
“Usimamizi wa rasilimali unakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi na mienendo mipya ya kibinadamu. Hali hizi zinahitaji fikra mpya, mbinu bunifu na suluhu zinazotekelezeka,” alisema.
Alisisitiza kwamba uongozi mpya unapaswa kuipa kipaumbele teknolojia za uchunguzi wa misitu, programu za urejeshaji uoto na kuimarisha ufadhili kwa uhifadhi unaoshirikisha jamii.
Kwa upande wake, Kilawe wa FAO aliwakumbusha wajumbe kuwa miaka ijayo itakuwa muhimu kwa Afrika kutokana na ongezeko la shinikizo la masoko ya kaboni, upotevu wa misitu na kupungua kwa makazi ya wanyamapori.
Baada ya kuchaguliwa, Jawara alianza rasmi majukumu yake kwa kuongoza mjadala wa tathmini ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kuandaa dira mpya ya usimamizi wa misitu kabla ya Mkutano wa FAO Kanda ya Afrika wa 2026.



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...