KAMPUNI ya Airtel Tanzania imetangaza kuendelea kwa ushirikiano wake na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kupitia utiwaji saini wa Awamu ya 10 ya ushirikiano wao, yenye lengo la kupanua huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini. Hafla ya utiliaji saini ilihudhuriwa na Mgeni Rasmi, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb).

Katika awamu hii mpya, Airtel Tanzania itajenga minara 132 kati ya 201 iliyopangwa kujengwa katika kata mbalimbali nchini. Hatua hii ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali unaowataka watoa huduma wote kuongeza upatikanaji wa huduma vijijini na kupunguza pengo la kimawasiliano.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, amewapongeza watoa huduma wa mawasiliano na kusema:

“Naipongeza Bodi na Menejimenti ya UCSAF kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana kwa ubora na kwa gharama nafuu. Pia nawapongeza watoa huduma wote kwa ushirikiano mkubwa mnaouonyesha kwa Serikali ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinaendelea kuwa bora, zenye tija, zinapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu kwa manufaa ya Watanzania.”

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Bw. Mohamed Hamis Abdullah, alisisitiza umuhimu wa mradi huu na kusema:

“Leo Serikali inashuhudia utiwaji saini wa mikataba ya ujenzi wa minara ya mawasiliano ya Awamu ya 10 katika kata 201 nchi nzima, kama ambavyo Mkurugenzi Mtendaji alieleza awali. Mradi huu ni muhimu na wa kimkakati, hivyo nichukue nafasi hii kuwapongeza watoa huduma wote wanaoshiriki.”

Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya utiliaji saini wa makubaliano, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Bw. Charles Kamoto, alisema:

“Ushirikiano wetu unaoendelea na UCSAF unaonyesha dhamira yetu thabiti ya kuchochea mageuzi ya kidijitali na kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana katika maeneo yote nchini. Kupitia mradi huu wa Awamu ya 10, Airtel itajenga 65% ya minara yote inayohitajika—sawa na minara 132 kati ya 201—ikiwa ni kielelezo cha kujitolea kwetu kuendeleza ujumuishaji wa huduma, kupanua mtandao, na kuwezesha jamii zaidi kunufaika na huduma za mawasiliano za kisasa.”

Airtel Tanzania imesisitiza upya dhamira yake ya kutoa huduma bora, za uhakika na za kisasa kwa Watanzania, kuhakikisha kwamba jamii za mijini na vijijini zinaendelea kunufaika na upanuzi wa mtandao wa mawasiliano.

Hatua hii ni mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali nchini na inadhihirisha nafasi ya uongozi ya Airtel Tanzania katika kuendesha upatikanaji jumuishi wa huduma za mawasiliano.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...