Na Diana Byera,Bukoba.

Diwani wa Kata ya Bakoba, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera Shabani Rashidi, ametangaza mkakati mpana wa maendeleo unaolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi, kuboresha elimu, kuimarisha huduma za afya na kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi katika nyumba za wananchi, sambamba na maelekezo ya kitaifa yanayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na mwandishi wa habari wa chombo hiki,Diwani Shabani alisema mkakati huo unajikita katika maeneo manne makuu, kukuza uchumi wa kaya, kuboresha mazingira ya kujifunzia katika shule za kata, kuongeza upatikanaji wa huduma rafiki za afya, na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa kwa kusukuma matumizi ya nishati safi ili kumtua mama mzigo wa kuni kichwani.

“Ninaamini maendeleo hayaji kwa maneno bali kwa mipango inayotekelezeka, Bakoba inahitaji uchumi wa kaya unaosimama, mazingira salama ya elimu, huduma za afya zinazowafikia wote, na mageuzi ya nishati safi ili kulinda afya za familia zetu na mazingira yetu, Huu ndio wajibu wangu, na sitarudi nyuma.” alisema Shabani

Katika eneo la uwezeshaji kiuchumi, Diwani huyo amekusudia kuanzisha programu za vikundi vya uzalishaji kwa vijana na kina mama, sambamba na fursa za mafunzo ya ujasiriamali na kuunganisha vikundi hivyo na taasisi za fedha zinazotoa mikopo yenye masharti rafiki.

Kwa upande wa elimu, mkakati huo unahusisha ukarabati wa miundombinu ya shule, uimarishaji wa madarasa, mabweni na vyoo, pamoja na kusimamia kwa karibu mahitaji ya walimu na wanafunzi ili kuinua kiwango cha ufaulu.

Kwenye huduma za afya, Diwani huyo alitaja mpango wa serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kujenga Zahanati ndani ya kata hiyo, kuimarisha vitengo vya mama na mtoto, na kufanya kampeni za uhamasishaji kuhusu lishe, chanjo na kinga ya magonjwa yanayoathiri jamii.

Aidha aliweka msisitizo maalum katika matumizi ya nishati safi, kuwa ameanza kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya kumtua mama mzigo wa kuni na kutumia Nishati safi ambapo alisema kuwa mpango huo umeanza kushika kasi katika kata hiyo kwa wananchi kutumia majiko ya Gesi ambapo Amesema ajenda iliyobaki ni kushauri serikali gharama za kujaza Gesi kupungua

Diwani huyo ambaye amemaliza miaka mitano na kuaminiwa tena, alisema kuwa mkakati huo unatarajiwa kuibadilisha Kata ya Bakoba kuwa eneo lenye uhai wa kiuchumi, maendeleo ya kijamii na mazingira salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...