Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Tanga na Wilaya ya Mkinga umezindua rasmi na kuendesha zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi wa kijiji cha Makota, kata ya Mwakijembe  wilayani Mkinga ili kupisha eneo tengefu la Mto Umba kujumuishwa ndani ya mpaka wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi leo Desemba 04, 2025.

Akizungumza na wanachi wa eneo hilo Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani amesema kuwa hatua hiyo iliyofikiwa kwa pande zote mbili itafungua milango kwa Mkoa wa Tanga kuwa na lango/malango yatakayopokea wageni na wawekezaji nje na ndani ya mipaka ya Tanzania ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi kupitia Wilayani Mkinga. 

"Lengo ni kuhakikisha uhifadhi endelevu ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi. Eneo hili la Mto Umba litafungua milango ya kuingia katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi na wageni wanavyokuja kulingana na ukuaji wa Utalii na Uhifadhi watapata fursa ya kutembelea vivutio vyetu na kuchangia pato la uchumi kwa zaidi ya 6.4% tulizokuwa tukizitengeneza hapo awalii"  amesema Mkuu wa Mkoa wa Tanga. 

Mkuu wa Mkoa aliongeza kuwa hatua hii itasaidia kupunguza na kudhibiti wanyamapori waharibifu hasa Tembo wanaoingilia makazi ya watu na mali zao na kuziharibu hususani msimu wa kilimo na kiangazi. 

"Niwasisitize ndugu zetu wa TANAPA kuendeleza jitihada za kukabiliana na wanyamapori hatarishi na sasa mmekabidhiwa vitendea kazi ikiwemo ndege nyuki zinazowasaidia kuwadhibiti wanyama hao".

Kwa upande wake Naibu  Kamishna wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kaskazini Steria Ndaga ameeleza kuwa kuna wananchi 115 wanahamishwa katika eneo hilo Tengefu na tathmini imekwisha kamilika na leo watalipwa ili kupisha eneo hilo litumike kwaajili ya shughuli za uhifadhi huku akitaja faida za eneo hilo tengefu kujumuishwa katika eneo la Hifadhi ya Taifa Mkomazi. 

"Eneo hili lina mandhari nzuri ya kuvutia watalii wa aina mbalimbali ikihusisha mimea, ndege na wanyamapori na tafiti mbalimbali zimefanyika na baadae kupitia serikali michakato mingi imefanyika ikaamua eneo hilo lihifadhiwe kwa faida kubwa za kitaifa" amesema Naibu Kamishna wa Uhifadhi. 

Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Mhe. Gilbert Kilima aliwashukuru wananchi wote na kuwapongeza kwa ushirikiano waliouonesha tangu mwanzo wa mchakato huu hadi mwisho. Amesisitiza kuwa  jukumu la uhifadhi ni la wananchi wote na kila mmoja ni mlinzi wa rasilimali za mataifa ikiwemo maliasili. 

Zoezi hilo la ulipaji fidia limesimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wilaya, viongozi wa serikali ya kata, kiijiji na kitongoji ili kuhakikisha kila mnufaika anapata fidia yake kama ilivyoratibiwa na wathamini wa zoezi hilo.
















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...