Na Pamela Mollel,Arusha
Jiji la Arusha limezindua rasmi Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji, hatua muhimu inayofungua ukurasa mpya wa uongozi na utawala katika jiji hilo. Uzinduzi huo umefanyika leo katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, ukihusisha shughuli zote za kikatiba ikiwemo uapisho wa madiwani, uchaguzi wa viongozi na uteuzi mbalimbali.
Katika uchaguzi uliofanyika, Maxmilian Matle Iranqhe amechaguliwa kuwa Meya wa Jiji la Arusha kwa ushindi wa kishindo baada ya kupata kura 33 kati ya kura 34, huku kura moja ikiwa ya hapana. Naye Julius W. Sekeyan (CCM) ameibuka kidedea katika nafasi ya Naibu Meya, akivuna kura 31 dhidi ya mpinzani wake Stanley Nathan (NLD) aliyepata kura 3. Matokeo hayo yametangazwa na Mwenyekiti wa muda wa uchaguzi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Dk. Jacob Rombo, ambaye alithibitisha kuwa jumla ya madiwani 34 walipiga kura.
Mara baada ya zoezi la uchaguzi kukamilika, madiwani wote 34—wakiwemo 25 wa kuchaguliwa na 9 wa viti maalum—waliapishwa kama sharti la kisheria linalowaruhusu kuanza kutekeleza majukumu yao rasmi. Uapisho huo umeweka msingi thabiti wa kuanza kwa awamu mpya ya utawala ndani ya jiji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Modest Mkude, amewataka madiwani kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za halmashauri pamoja na kutekeleza kiapo chao kwa vitendo. Amehimiza ushirikiano baina ya madiwani na watendaji, akiwataka kuondokana na chuki, ubinafsi na kuweka mbele maslahi ya wananchi.
Mkude amesisitiza kuwa uongozi bora wa jiji lenye kasi kubwa ya ukuaji kama Arusha unahitaji umoja, uwajibikaji na utulivu. Amebainisha kuwa misingi hiyo ndiyo itakayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi na kwa wakati.
Kwa mujibu wa ratiba, Baraza jipya la Jiji la Arusha linatarajiwa kuanza vikao vyake rasmi muda mfupi ujao. Vikao hivyo vitatoa nafasi ya kuanza kupanga ajenda za awali za maendeleo, kupitia mikakati ya usimamizi wa huduma za jamii, pamoja na kuweka mwelekeo wa utekelezaji wa miradi mipya na inayoendelea.
Uzinduzi huu unaiweka Arusha kwenye njia ya awamu mpya ya uongozi unaotazamiwa kuleta mabadiliko chanya, uwazi na kasi katika utendaji wa halmashauri, huku wananchi wakitarajia kuona maboresho zaidi kwenye huduma, miundombinu na usimamizi wa rasilimali za jiji.


.jpeg)





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...