Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Zanzibar itaendelea kuwakaribisha wawekezaji wengi zaidi, kwani bado ina fursa nyingi za uwekezaji zinazohitaji ushirikiano wa wadau na taasisi za kimataifa.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 01 Desemba 2025 alipokutana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Commonwealth Enterprise and Investment Council, Lord Swire, na ujumbe wake waliofika Ikulu kwa mazungumzo.
Rais Dkt. Mwinyi ameuambia ujumbe huo kuwa Zanzibar imekuwa ikifanya juhudi kubwa katika kuimarisha sekta ya uwekezaji kwa lengo la kuvutia wawekezaji hususan katika sekta mbili kuu za uchumi, ambazo ni Uchumi wa Buluu na Utalii.
Ameeleza kuwa ujio wa ujumbe huo ni fursa muhimu kwa Zanzibar katika kufanikisha malengo ya uwekezaji.
Amezitaja sekta za Uchumi wa Buluu na Utalii kuwa ndizo sekta kuu zinazochangia takribani asilimia 30 ya pato la taifa, na kwamba bado kuna fursa nyingi ambazo taasisi hiyo inaweza kushirikiana na Zanzibar.
Aidha, ameuhakikishia ujumbe huo kuwa Zanzibar imejipanga vizuri kubainisha fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali pamoja na maeneo ambayo bado yanahitaji wawekezaji katika biashara na uwekezaji.
Akizungumzia Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Dkt. Mwinyi amesema kuwa eneo hilo ni la kimkakati na lina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta tofauti ikiwemo usafirishaji, mafuta na gesi, na biashara.
Ameongeza kuwa Serikali ina matarajio ya kuwakaribisha wawekezaji wengi zaidi kuwekeza katika eneo hilo.
Naye Mwenyekiti wa Commonwealth Enterprise and Investment Council, Lord Swire, amesema kuwa Zanzibar ni mshirika muhimu, na kwamba taasisi hiyo iko tayari kushirikiana nayo katika nyanja mbalimbali za ushirikiano, uwekezaji na biashara kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi.
Taasisi ya Commonwealth Enterprise and Investment Council inajishughulisha na kuimarisha ushirikiano, biashara na uwekezaji miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.










Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...