Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa wito kwa taasisi na wadau wa sekta ya utalii kuongeza ushirikiano ili kuhakikisha Tanzania, ikiwemo Zanzibar, inaendelea kunufaika na tuzo na fursa za kimataifa katika sekta ya utalii.
Rai hiyo imetolewa leo tarehe 12 Desemba 2025, Ikulu Zanzibar, baada ya Rais Dkt. Mwinyi kupokea Tuzo ya Africa’s Best Corporate Retreat Destination 2025, ambayo Zanzibar imeshinda kwenye Mashindano ya Dunia ya Utalii wa Safari (World Travel Awards 2025) yaliyofanyika nchini Bahrain.
Tuzo hiyo imewasilishwa kwa Rais na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Hamad Hassan Chande. Ushindi huo ni wa kwanza kwa Zanzibar, baada ya kushindana na mataifa manne: Kenya, Afrika Kusini, Morocco na Botswana.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amesema ushindi huo ni heshima kubwa kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, na unadhihirisha kiwango kikubwa cha maendeleo ya sekta ya utalii nchini. Amesisitiza umuhimu wa kuongeza ubora wa huduma, kuimarisha vivutio vya utalii, na kutumia tuzo hizo kama chachu ya kushindana kimataifa, hasa katika eneo linalokua kwa kasi la utalii wa mikutano na matukio.
Ameeleza kuwa utalii ni “sekta mama” ya uchumi wa Zanzibar, hivyo mipango thabiti na ushirikiano wa karibu miongoni mwa wadau inahitajika ili kuongeza thamani na mapato yatokanayo na sekta hiyo. Aidha, ametumia nafasi hiyo kuhimiza maandalizi ya pamoja kuelekea Tanzania kuwa mwenyeji wa World Travel Awards Grand Final 2026, akiwataka wadau waongeze ubunifu na kuboresha bidhaa na huduma za utalii.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Chande amesema ushindi wa Zanzibar ni hatua kubwa inayoliweka taifa katika ramani ya dunia kama kitovu kipya cha utalii wa safari barani Afrika. Amebainisha kuwa Tanzania imeibuka na tuzo tano kwenye mashindano hayo, ikiwemo tuzo kubwa ya Tanzania World’s Leading Safari Destination.




.jpeg)







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...