SERIKALI ya Awamu ya Sita imeahidi kuendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya uchukuzi ili kuhakikisha Taifa linakuwa na miundombinu imara pamoja na wataalam mahiri watakaosimamia na kuendesha miradi mikubwa ya maendeleo nchini.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ametoa ahadi hiyo leo Desemba 19, 2025, katika Mahafali ya 41 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) yaliyofanyika katika viwanja vya chuo hicho jijini Dar es Salaam.

Prof. Mbarawa amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya uchukuzi ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), bandari, viwanja vya ndege, barabara, madaraja pamoja na ununuzi wa meli na ndege, hali inayoongeza mahitaji ya wataalam wabobezi katika sekta hiyo.

Amesema NIT imeendelea kuwa taasisi muhimu katika kuandaa rasilimali watu yenye sifa stahiki, hususan katika maeneo ya kimkakati ya usafiri wa reli, maji na anga, huku idadi ya wahitimu ikiendelea kuongezeka sambamba na maboresho ya miundombinu ya chuo.

“Uwekezaji huu mkubwa wa Serikali unahitaji wataalam wa kutosha na wenye weledi. Ndiyo maana Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kina nafasi kubwa sana katika safari ya maendeleo ya nchi yetu,” alisema Prof. Mbarawa.

Waziri Mbarawa amebainisha kuwa Serikali imeongeza ndege tatu kwa ajili ya mafunzo ya urubani, kuanza kwa ujenzi wa Kampasi ya Kilimanjaro pamoja na kufikia hatua za mwisho za kumpata mkandarasi wa Kampasi ya Lindi, hatua zinazolenga kupanua wigo wa mafunzo na kuongeza fursa kwa Watanzania.

Aidha, ameipongeza NIT kwa kuanza kutoa mafunzo ya urubani nchini, hatua itakayopunguza gharama kwa Watanzania waliokuwa wakilazimika kusoma nje ya nchi, na kuhimiza chuo kuendelea kuwekeza katika teknolojia na ubunifu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi duniani.

Pia Prof. Mbarawa amewataka wahitimu kuwa wazalendo, kulinda amani ya nchi na kuendelea kujiongezea maarifa ili kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa, akisisitiza kuwa bila amani hakuna maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la NIT, Profesa Ulingeta Mbamba, alisema chuo kitaendelea kuboresha ubora wa mafunzo ikiwemo kuimarisha rasilimali watu, kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kukuza uchumi shindani na endelevu.

Alisema chuo kinatekeleza Mpango Mkakati wa miaka 2020/21–2025/26 unaolenga kuzalisha wataalamu katika nyanja tano za usafirishaji, ikiwemo anga, reli na usafiri wa majini, kwa maslahi mapana ya Taifa.

Naye Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Profesa Prosper Mgaya, alisema jumla ya wahitimu 4,121 wamehitimu kuanzia ngazi ya cheti hadi uzamili, ambapo asilimia 38.9 ni wanawake, sawa na ongezeko la asilimia tano ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Alisema uwekezaji mpya wa Serikali katika maeneo mbalimbali ya mafunzo umewezesha kupungua kwa gharama za baadhi ya kozi, hususan kozi ya urubani. Aliongeza kuwa kwa mara ya kwanza Serikali imekiwezesha chuo kutoa mafunzo ya urubani na ufundi wa ndege hapa nchini.

“Kwa sasa tuna wanafunzi wa urubani 22; kati yao 10 wamekamilisha mafunzo ya ground school na saba wako katika hatua ya mafunzo ya solo. Mwezi wa pili mwakani tunatarajia kushuhudia wahitimu wa kwanza wa kozi ya urubani,” alisema Prof. Mgaya.

Aliongeza kuwa uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya usafirishaji, ikiwemo kuongezeka kwa ndege za Shirika la Ndege la Taifa hadi kufikia 16, ukarabati wa meli na miundombinu mingine, umeongeza mahitaji ya wataalamu, hali iliyosababisha NIT kuongeza udahili kwa asilimia 35.6.

Aliwakumbusha wahitimu kuwa mafanikio yao hayatapimwa kwa ufaulu wa mitihani pekee, bali kwa viwango vya taaluma, maadili na ufanisi wa utendaji wao kazini.







Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...