Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma tarehe 15 ilifanya ziara ya kikazi kumfikia mjasiriamali Idrisa Aclay Chisigwa wa Wilaya ya Bahi, kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zake za kikodi kufuatia malalamiko aliyoyawasilisha. Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za TRA kuhakikisha walipa kodi wanapata uelewa sahihi wa masuala ya kodi na kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Katika ziara hiyo, maafisa wa TRA walitembelea biashara ya mjasiriamali huyo iliyopo Bahi pamoja na tawi lake lililopo Manyoni, ambapo walijionea shughuli za kibiashara na kufanya mazungumzo ya kina kuhusu masuala ya kodi. Kupitia mazungumzo hayo, TRA ilitoa elimu kuhusu wajibu wa kikodi unaohusiana na biashara zake pamoja na utaratibu wa malipo ya kodi kwa awamu, kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyopo.

Kupitia majadiliano hayo, TRA ilitoa ufafanuzi wa kina uliolenga kuongeza uelewa sahihi wa mjasiriamali kuhusu mfumo wa kodi kwa ujumla na namna ya kutimiza wajibu wake kwa usahihi. Elimu hiyo ilisaidia kuondoa dhana potofu zilizokuwepo na kuweka msingi wa uelewa mzuri utakaomuwezesha kuendesha biashara yake kwa kuzingatia matakwa ya kisheria.

Mjasiriamali Idrisa Aclay Chisigwa aliishukuru TRA kwa kumtembelea na kutoa elimu hiyo, akibainisha kuwa elimu ya kodi ni muhimu kwa vijana wengi wanaojihusisha na biashara. Alieleza kuwa vijana wengi hushindwa kutimiza wajibu wao wa kikodi kutokana na kukosa taarifa sahihi. Ameahidi kuwa Balozi mzuri wa masuala ya kodi Mkoa wa Dodoma kwa kuwahamasisha vijana wengine kujisajili biashara zao, kupata elimu sahihi ya kodi na kulipa kodi kwa wakati.

TRA inaendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya walipa kodi na mamlaka husika katika kujenga mazingira rafiki ya biashara, kukuza uchumi na kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya kikodi unafanyika kwa uelewa, uwajibikaji na hiari. Tunawashukuru, Tunaendelea kuwasikiliza na kuwezesha Biashara zenu, Pamoja tunajenga Taifa letu.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...